Jun 30, 2024 11:13 UTC
  • New York Times, Gazeti la kwanza la Marekani kumtaka Biden ajiondoe katika uchaguzi wa rais 2024

Gazeti la New York Times limekuwa gazeti la kwanza la Marekani kumtaka rais aliyeko madarakani, Joe Biden, kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa 2024 kufuatia utendaji dhaifu katika mdahalo dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump siku chache zilizopita.

Biden, Mdemokrati na Trump, Mdemokrati wa zamani aliyegeuka Republican, walikutana katika mdahalo Alkhamisi usiku katika makao makuu ya CNN huko Atlanta, bila watazamaji wa moja kwa moja.

Katika duru ya kwanza ya midahalo ya kabla ya uchaguzi ujao wa rais unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, wateule hao watarajiwa kuwakilisha vyama viwili vikuu vya Marekani katika uchaguzi huo, walibishana kuhusu uchumi wa Marekani, sera ya kigeni, COVID, uavyaji mimba na uhamiaji, huku wakirushiana matusi ya nguoni, na kutaja majina watu wa familia zao, masuala ya maadili, na hata kila mmoja wao kumpa changamoto mpinzani wake kwenye mechi ya golfu.

Ijumaa iliyopita siku moja tu baada ya mdahalo huo, bodi ya wahariri ya NYT ilimtaka Biden, 81, ajiondoe katika kinyang'anyiro cha kutaka kubakia White House.

Biden na Trump katika mdahalo wa urais

Walisema Wademokrati wanahitaji kupata mgombea bora kuchukua nafasi ya Biden.

Wito huo ilitolewa baada ya waangalizi wa mdahalo wa urais kusema Biden alionekana dhaifu na aliyechanganyikiwa, akijitahidi kumaliza sentensi zake na kuchanganya maneno wakati akizungumza.

Bodi ya wahariri ilihitimisha kuwa Wanademokrati wana nafasi nzuri ya kushinda dhidi ya Trump iwapo Biden atapata mbadala na kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.