Jul 02, 2024 02:59 UTC
  • IOM: Wahamiaji 303 waliokamatwa Libya wamerejeshwa walikotoka katika kipindi cha wiki moja

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitangaza jana Jumatatu kwamba, jumla ya wahamiaji haramu 303 waliokamatwa nchini Libya wamereshwa katika nchi zao za asili kwenye kipindi cha wiki moja iliyopita wakiwemo Wabangladeshi 162.

Shirika hilo limesema kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Wiki iliyopita, IOM nchini Libya iliwezesha safari mbili za kukodi ndege za Voluntary Humanitarian Return (VHR), kupeleka wahamiaji 162 kutoka Benghazi hadi Dhaka Bangladesh na wahamiaji 141 kutoka Tripoli hadi Guinea Bissau na Benin." 

Wahamiaji hao walirejeshwa makwao kutokea Libya chini ya mpango wa VHR wa shirika hilo la uhamiaji la IOM, ambao lengo lake ni kuwasaidia kurejea makwao wahamiaji waliokwama nchini Libya.

Tamaa mbele mauti nyuma, tamaa chapwa ya kupata maisha bora Ulaya inawasababishia baadhi ya vijana wa Afrika na nje ya Afrika kuhatarisha maisha yao na kupoteza maisha kwenye mawimbi makali ya Bahari ya Mediterania

 

Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa la uhamiaji, wahamiaji 226, wakiwemo wanawake 32 na watoto 13, walikamatwa nje ya pwani ya Libya katika kipindi cha baina ya taarehe 23 hadi 29 mwezi ulioisha wa Juni, 2024.

Taarifa ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM vile vile imesema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wahamiaji 8,980 wamekamatwa na kurejeshwa Libya. 358 kati yao wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 513 wametoweka kwenye pwani ya Libya na hawajapatikana hadi hivi sasa.

Tangu ulipoangushwa utawala wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi mwaka wa 2011, nchi hiyo imekuwa mahali pazuri pa kuondokea baadhi ya wahamiaji wa mataifa mbalimbali hasa ya Afrika wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kwa tamaa kidhabi na chapwa ya kupata maisha bora barani Ulaya.