Jun 30, 2024 11:12 UTC
  • Utafiti wa Israel: Nguvu zetu za kijeshi zinafifia na vita na Lebanon ni maafa

Utafiti uliotayarishwa na Taasisi ya Utafiti wa Usalama wa Taifa ya Israel katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv umetahadharisha kuhusu hatari ya kuingia katika makabiliano makubwa ya kijeshi na harakati ya Hizbullah ya Lebanon, na kusisitiza kuwa, kuendelea kuwepo Israel kama taifa kumeingia mashakani, na taswira yake kama taifa lenye nguvu za kijeshi inafifia.

Katika nakala ya muhtasari wa utafiti huo, Meja Jenerali mstaafu, Tamir Heyman, kiongozi wa taasisi hiyo na mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Israel (AMAN), amehoji uwezekano wa Israel kupanua vita huko Lebanon, akisema kuwa "kuhamishia vita huko kaskazini kabla ya kumaliza vita vya Gaza ni jambo lisilofaa, na kunaweza kusababisha vita vya muda mrefu vya kuzidi kuidhoofisha Israel.

Meja Jenerali mstaafu amesisitiza kuwa vita vya Gaza vimeifanya Israel ikabiliwe na tishio la kutengwa kimataifa, baada ya wengi katika uga wa kimataifa kuanza kuiona kama mchokozi na katili.

Heyman ameongeza kuwa, Hizbullah ina miundombinu na uwezo wa kijeshi wa kupigana vita vya muda mrefu sana ambavyo vitasababisha uharibifu mkubwa kwa Israel.

Silaha za Hizbullah ya Lebanon

Utafiti huo unatazamia kuwa Hizbullah itarusha maelfu ya makombora na maroketi kila siku na kwa muda mrefu endapo vita vikali vitazuka, na kueleza kuwa haitawezekana kuyazuia yote, hasa kwa vile baadhi ya makombora hayo yatarushwa kutokea maeneo mengine kama Iran, Iraq, Syria, na Yemen; na hii ni hatari ya kijeshi na kwa raia ambayo Israel haijawahi kushuhudia.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inasema itaendeleza mashambulizi dhidi ya vituo vya jeshi la Israel hadi utawala huo utakaposisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.