Jun 29, 2024 02:25 UTC
  • Serikali ya Biden yakiri kudumisha siasa za vikwazo dhidi ya Iran

Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano sambamba na siasa za undumakuwili za Washington kuhusu wananchi wa Iran, kwamba nchi hiyo ya imeweka vikwazo zaidi ya 600 dhidi ya serikali na mashirika ya Iran.

Tarehe 25 Juni 2024, Wizara ya Fedha ya Marekani iliweka vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi na mashirika 50 katika hatua yake ya karibuni kabisa dhidi ya Iran, kwa madai kwamba mashirika na watu hao wameunda mtandao mkubwa wa siri wa kibenki, wana uhusiano na Mapinduzi ya Kiislamu na pia na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumzia vikwazo hivyo, Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema hiyo ni sehemu ya vita vya kiuchumi ambavyo Marekani imekuwa ikivitekeleza kidhalimu dhidi ya wananchi wa Iran. Amesema pamoja na hayo lakini Wairani wanaendelea kusimama imara dhidi ya vikwazo na kwamba lililo muhimu katika vita hivi vya kiuchumi ni 'nguvu ya irada na sio nguvu ya kutekeleza vikwazo.'

Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye katika kampeni zake za uchaguzi alidai kutekeleza siasa huru zilizo kinyume na sera za Donald Trump rais wa zamani wa nchi hiyo kuhusu Iran, amekuwa akitekeleza siasa hizo hizo tangu mwanzo wa utawala wake, yaani Januari 2021, siasa ambazo zimetajwa kuwa ni za vikwazo za kulemaza na mashinikizo ya juu zaidi ya serikali ya Washington dhidi ya Tehran. Bila ya kutaja ni serikali gani ilijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kinyume cha sheria, Biden amekuwa akidai kuwa Marekani itarejea katika mapatano hayo iwapo Iran itatekeleza kikamilifu ahadi zake zote ilizotoa katika mapatano hayo. Bila shaka siasa za Biden ni siasa zile zile za mtangulizi wake Trump ambaye alitumia wakati wake mwingi kutaka kuilazimisha Iran ipige makoto mbele ya Marekani na kutekeleza matakwa yake yakiwemo ya kutotengeneza makomora ya masafa marefu wala kujiimarisha kisiasa katika eneo la Asia Magharibi.

Vikwazo vya Wamagharib dhidi ya Iran

Licha ya siasa hizo za uhasama za Marekani dhidi ya Iran lakini akizungumza katika kikao cha Seneti ya Marekani, mnamo Mei 21, mwaka huu, Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo alikiri kwamba tangu utawala wa Biden uchukue madaraka, umeweka zaidi ya vikwazo 600 dhidi ya watu binafsi na taasisi za kifedha za Iran, lakini hatua hiyo haijaweza kuizuia nchi hii kuuza nje mafuta yake.

Suala jingine muhimu ni kwamba Marekani imeweka vikwazo vingi zaidi dhidi ya nchi nyingine za dunia katika kipindi cha karne mbili zilizopita. Kwa hakika, matumizi ya vikwazo yamekuwa sehemu muhimu ya sera za kigeni za Marekani. Mnamo Oktoba 18, 2022, Wizara ya Fedha ya serikali ya Biden, baada ya miezi kadhaa ya kukagua mfumo wa vikwazo, ilichapisha ripoti iliyoonyesha kwamba, kama zilivyokuwa serikali za zamani za Marekani, serikali hiyo inavichukulia vikwazo kama zana muhimu ya kuendeleza kile kinachodaiwa kuwa ni kulinda masilahi ya kitaifa ya Marekani na hata kutaka kuiboresha zaidi. Gazeti la The Hill pia liliripoti mnamo Oktoba 22, 2022, kuwa vikwazo dhidi ya watu na nchi zingine vinachukuliwa kuwa zana muhimu ya sera za kigeni za Marekani ambapo vikwazo hivyo vimeongezwa mara 10 katika miongo 2 iliyopita.

Hata hivyo, kutokana na kupungua taratibu kwa nguvu za Marekani na mabadiliko katika mfumo wa kisiasa na kiuchumi duniani hususan katika miongo miwili iliyopita, athari za vikwazo hivyo zinatiliwa shaka pakubwa. Jarida la Wall Street Journal katika ripoti yake ya karibuni limesema vikwazo vya Magharibi na udhibiti wa mauzo ya nje unasimamiwa na Washington kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa Marekani, lakini si tu jambo hilo halijafanikiwa, bali pia limepelekea nchi zilizowekewa vikwazo kuungana kisiasa na kiuchumi na kuunda kambi mpya ya kiuchumi dhidi ya Marekani. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kambi ya nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani sasa kwa pamoja ina uchumi mkubwa wa kutosha kuzilinda kutokana na vita vya kifedha vya Washington, zikifanya biashara ya kila kitu kuanzia ndege zisizo na rubani na makombora hadi dhahabu na mafuta.

Tags