Jul 01, 2024 02:23 UTC
  • Iran ni namba moja Ulimwengu wa Kiislamu katika uzalishaji wa sayansi na teknolojia

Kwa mujibu wa hifadhidata ya kimataifa ya "Web of Science," Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya sita duniani na ya kwanza kati ya nchi za Kiislamu katika uzalishaji wa sayansi na teknolojia ya mtandao wa neva.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sayyid Ahmed Fazelzadeh, Mkuu wa Taasisi ya Utoaji na Ufuatiliaji ya Sayansi na Teknolojia ya Ulimwengu wa Kiislamu (ISC) akisema hayo jana Jumapili na huku akitangaza viwango vipya vya kimataifa vya uzalishaji wa sayansi ya teknolojia duniani amesema kuwa Iran imezidi kuimarika katika upande huo kiasi kwamba hivi sasa inashika nafasi ya kwanza kati ya nchi za Ulimwengu wa Kislamu katika uzalishaji wa sayansi na teknolojia ya mtandao wa neva.

Sayyid Ahmed Fazelzadeh, Mkuu wa Taasisi ya Utoaji na Ufuatiliaji ya Sayansi na Teknolojia ya Ulimwengu wa Kiislamu (ISC)

 

Mkuu wa Taasisi ya Utoaji na Ufuatiliaji ya Sayansi na Teknolojia ya Ulimwengu wa Kiislamu yenye makao yake huko Shiraz, makao makuu ya mkoa wa Fars wa kusini mwa Iran, ameongeza kuwa, akili mnemba (Artificial Intelligence) ni elimu pana yenye matawi mengi yakiwemo ya kompyuta ya kuona, usindikaji wa lugha asilia, kujifunza kwa kutumia mashine, robotiki, mitandao ya neva na kadhalika.

Vile vile amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mwanzoni mwa safari yake katika uga huo na kwamba maendeleo yaliyosababishwa na mapinduzi ya nne ya kiviwanda ulimwenguni, hayajafikia kiwango kinachotakiwa. 

Mkuu huyo wa Taasisi ya Utoaji na Ufuatiliaji ya Sayansi na Teknolojia ya Ulimwengu wa Kiislamu aidha amesema, kuhakiki na kuchambua nafasi ya kisayansi katika teknolojia na matawi ya akili mnemba katika viwango vya kimataifa ni jambo muhimu sana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanyia kazi nyuga hizo.

Tags