Nov 30, 2023 14:48 UTC
  •  Iran kuzalisha zaidi ya dawa 60 za radiopharmaceuticals

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) limepokea agizo la kuzalisha zaidi ya dawa 60 za radiopharmaceuticals kwa ajili ya soko la ndani.

Msemaji wa shirika hilo,  Behrouz Kamalvandi amesema Shirika la Nishati ya Atomiki limetoa msaada mkubwa kwa sekta ya afya katika miaka ya hivi karibuni.

Amebainisha kuwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limetia saini mkataba na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Wizara ya Afya ili kuzalisha dawa mpya 66 za radiopharmaceuticals.

Aidha amesema dawa za radiopharmaceuticals zilizotegenezwa nchini Iran kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya saratani hutengenezwa kwa ubora wa kiwango cha kimataifa.

Mnamo Desemba 2022, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alisema Iran inalenga kuwa kitovu cha kimataifa cha utengenezaji dawa za deuterium.

Amesema: "Katika siku za usoni zisizo mbali sana tutageuka kuwa kitovu cha kutengeneza dawa kulingana na deuterium ambayo ni mbadala mzuri wa dawa za kemikali na kiwango cha madhara ni cha chini sana kwa mtumizi."

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran lilizindua awamu ya pili ya kitengo chake cha uzalishaji wa deuterium katika Kituo cha Afya cha Arak Heavy Water Reactor katikati mwa Iran mwezi Aprili 2021.

@@@

Maonyesho ya 18 ya Kimataifa ya Tiba, Matibabu ya Meno, Vifaa vya Maabara na Viwanda Vinavyohusiana yamefanyika hivi karibuni katika mji wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran.

Maonyesho hayo ambayo yalichukua muda wa siku nne yalionesha vifaa vya matibabu pamoja na vifaa vya upasuaji na maabara miongoni mwa masuala mengine. Kwa mujibu wa Saeed Seifi, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Maonyesho cha Kimataifa cha Mashhad, Mkoa wa Khorasan Razavi kampuni 80 kutoka kote Iran pamoja na Afghanistan, Iraq na Pakistan zilishiriki katika hafla hiyo.

Maonyesho hayo yalilenga kutambulisha teknolojia za kisasa na uwezo wa wanaviwanda wanaofanya kazi katika uwanja wa uhandisi wa matibabu katika viwango vya kitaifa na kimataifa, na kuongeza ushirikiano kati ya wazalishaji nchini Iran, nchi jirani, Asia ya Kati na Ghuba ya Uajemi.

@@@

Kampuni moja ya Iran  inayojikita katika maarifa na utafiti imeunda mashine ya CT scan ambayo hugharimu dola laki mbili kuagizwa kutoka nje ya nchi $200,000.

Mashine hiyo iliyotengenezwa na Shirika la Behyaar Sanaat Sepahan itaanza kutumika hivi karibuni katika vituo vya afya kote nchini.

Farid Nejatbakhsh-Azadani, Mkurugenzi Mtendaji wa Behyaar Sanaat Sepahan anasema: "Bidhaa hii inaweza kutumika katika uwanja wa utambuzi wa maradhi na katika matibabu katika tiba ya mionzi au radiotherapy."

Wahandisi wa Behyaar Sanaat Sepahan wametumia muda wa miaka minane kuunda mashine hiyo ya CT scan na asilimia 85 ya vipuri vyake ni vya ndani ya nchi.

Kifaa hicho kinaashiria hatua kubwa katika kufikia kujitosheleza, kukuza hadhi ya kisayansi ya Iran katika eneo na dunia kwa kuigeuza nchi kuwa mojawapo ya nchi 10 pekee zinazomiliki teknolojia hiyo ya uzalishaji wa CT Scan duniani.

@@@

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewekwa miongoni mwa nchi tano bora katika Olympiadi za kimataifa huku wanafunzi wa Iran wakipata mafanikio makubwa katika nyanja na mashindano mbalimbali ya kisayansi kote duniani.

Elham Yavari, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukuza Vipaji Bora linalojulikana kama SAMPAD, amesema Iran ni kati ya nchi tano bora ulimwenguni katika Olympiads za kimataifa.

Yavari ameashiria mpango wa mageuzi ulioidhinishwa na Wizara ya Elimu ya Iran mwaka 2011 ambao ulifafanua matarajio ya miaka 20 ya kuinua viwango vya elimu na uboreshaji wa mfumo wa elimu nchini kote.

Mkuu huyo wa SAMPAD amesema mpango huo uliopewa jina la Hati ya Marekebisho ya Msingi, unaelimisha wanafunzi katika nyanja sita za michezo, sayansi, ujasiriamali na uchumi, jamii, dini na utamaduni.

"Waraka huo unaitaka Wizara ya Elimu kutoa mafunzo kwa wanafunzi katika nyanja zote na kukuza vipaji vyao," Yavari alisema na kuongeza, "Mfumo wa elimu wa nchi nyingine ni bora, lakini Iran ni miongoni mwa nchi tano bora duniani katika Olimpiadi za Kisayansi."

Mnamo Agosti, wanafunzi wa Iran walishinda nafasi ya tatu katika Olympiad ya 16 ya Kimataifa ya Astronomia na Astrofizikia huko Silesia, Poland.

Uingereza ilishinda nafasi ya kwanza ya mashindano hayo kwa medali tano za dhahabu na India ilimaliza ya pili ikiwa na dhahabu nne na moja ya fedha.

Mwezi mmoja kabla, wanafunzi wa Iran walishinda medali sita katika Olympiad ya 64 ya Kimataifa ya Hisabati, ambayo iliandaliwa na mji wa Japan wa Chiba.

Timu ya wanafunzi ya Iran pia ilijishindia medali tano kwenye Olympiad ya 53 ya Kimataifa ya Fizikia iliyoandaliwa na Tokyo mnamo Julai.

@@@

Ili kukomesha kukithiri kwa taarifa potofu na kauli za chuki mitandaoni ambazo ni “tishio kubwa kwa utulivu na mshikamano wa kijamii” Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limezindua mpango kazi wa kudhibiti majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, amesema mpango kazi huo ni matokeo ya mchakato wa mashauriano kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, huku michango zaidi ya 10,000 kutoka nchi 134 ikikusanywa katika kipindi cha miezi kumi na minane iliyopita.

“Teknolojia ya kidijitali imewezesha maendeleo makubwa kwenye uhuru wa kujieleza. Lakini majukwaa ya mitandao ya kijamii pia yameongeza kasi na kuzidisha uenezaji wa taarifa za uongo na matamshi ya chuki, na kusababisha hatari kubwa kwa mshikamano wa jamii, amani na utulivu. Ili kulinda ufikiaji wa habari, lazima tudhibiti majukwaa haya bila kukawia, wakati huo huo tukilinda uhuru wa kujieleza na haki za binadamu.”

Mpango kazi huo wenye zaidi ya kurasa arubaini, unaeleza kanuni zinazopaswa kuheshimiwa pamoja na hatua madhubuti zinazopaswa kutekelezwa na wadau wote ambao ni serikali, mamlaka za udhibiti, asasi za kiraia na majukwaa yenyewe.

@@@

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania  Omar Kipanga amesema serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi za Elimu ya Juu nyanja ya tehama ili kusaidia kuzalisha wataalamu wengi na mahiri watakaosaidia maendeleo ya uchumi wa kidigitali.
Mhe. Kipanga alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Arusha wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 6 ya Kituo cha Umahiri katika TEHAMA cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM AIST), ambapo amesema ustawi wa baadaye wa uchumi wa Afrika utategemea kiwango cha uwekezaji katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi.

‘’Suala la ubunifu litaendelea kuwa muhimu katika ukuaji wa uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na usafirishaji, katika miongo ijayo uwezo wa uvumbuzi ni muhimu kwa ajili ya ushindani kitaifa na kimataifa’’ alisema Mhe. Kipanga.


Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imewajibika kikamilifu katika kufanya uwekezaji mkubwa kwanza kwenye miundombinu, kusomesha wataalamu mbalimbali lakini pia katika kuhakikisha inaandaa bajeti ambayo itawezesha masuala ya tehama kutumika kwa ufanisi.

Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio Kipanyula alisema tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho wameweza kuzalisha wahitimu 136 ambao wanatoka katika nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Prof. Kipanyula amesema kituo hicho kinajivunia mafanikio makubwa ikiwemo kutoa ufadhili kwa Wanafunzi wote katika nchi za Afrika Mashariki kusoma katika Taasisi yao.

 

 

 

Tags