Mafanikio makubwa ya nyuklia ya Iran
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojai nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.
Rais Masoud Pezeshkian ametembelea maonyesho ya mafanikio ya nyuklia huku Iran ikiadhimisha Siku yake ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia kwa kuzindua bidhaa nane.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Mohammad Eslami, pamoja na kundi la maafisa waandamizi waliandamana na Rais Pezeshkian katika ziara yake katika shirika hilo mjini Tehran tarehe 9 Aprili.
Maonyesho hayo yanaonyesha mafanikio ya Iran katika mzunguko wa mafuta ya nyuklia, uzalishaji wa nishati na umeme, uzalishaji wa maji mazito na bidhaa zake, madawa ya nyuklia (radiopharmaceuticals), teknolojia ya plasma, matumizi ya mionzi, na teknolojia nyingine za kisasa zinazohusiana.
Maonyesho hayo yanajumuisha mabanda yanayoonyesha mafanikio ya ndani katika nyanja za jiografia ya anga kwa kutumia ndege (airborne geophysics), miradi ya uchunguzi na uendeshaji wa migodi ya urani, uzalishaji wa “keki ya njano,” usindikaji wa urani, utengenezaji wa vijisahani vya mafuta (pellets) na mitambo ya mafuta, pamoja na mchakato wa kurutubisha urani.
Sehemu moja ya maonyesho hayo imetengwa kwa ajili ya kuonesha miradi inayohusiana na mitambo ya umeme ya nyuklia, ikijumuisha maendeleo ya ujenzi wa Mitambo ya Bushehr Awamu za 2 na 3, ripoti ya kiwango cha uzalishaji umeme wa Kituo cha Bushehr Awamu ya 1, ambacho ni kituo cha kwanza cha nyuklia cha Iran, ripoti ya ujenzi wa Kituo cha Nyuklia cha Karoun, pamoja na usanifu na utengenezaji wa vipuri vinavyohitajika kwa ajili ya mtambo wa Bushehr.
Sehemu nyingine imejikita katika uzalishaji wa maji mazito na misombo ya deuteriamu, uzalishaji wa madawa ya nyuklia, vifaa vya vipimo vya nyuklia, maendeleo ya teknolojia ya plasma, matumizi ya mionzi katika tiba na kilimo, mionzi ya damu, utengenezaji wa viharakisha viwandani (industrial accelerators), na teknolojia mpya kama quantum na teknolojia za quantum.
Katika sherehe hiyo ilibainika kuwa Iran imekuwa nchi ya pili duniani kutengeneza kibiashara isotopu ya mionzi ya Rhenium-188, ambayo hutumika katika matibabu ya saratani, na hivyo kuvunja ukiritimba wa Ujerumani katika uzalishaji wake.
Krimu mpya ya ngozi yenye Rhenium-188 (Re-188), inatoa suluhisho la kisasa kwa ajili ya kutibu saratani za ngozi za kawaida.
Rhenium-188 ni isotopu ya mionzi inayotoa chembe za beta zenye nishati kubwa jambo linaloifanya kuwa chaguo la kipekee na lenye matumaini makubwa katika tiba za nyuklia.
Hadi sasa, Ujerumani ilikuwa ikitambulika kama mtengenezaji pekee wa kibiashara wa Rhenium-188, lakini Iran imevunja ukiritimba huo na kuwa nchi ya pili kuzalisha wakala huyu wa dawa ya mionzi kwa ajili ya matumizi ya matibabu.
Katika sekta ya afya, dawa nyingine mbili bunifu za mionzi zilitangazwa katika hafla hiyo ambazo ni: Gallium FAPI, inayotumika kugundua zaidi ya aina 30 za saratani, na Lutetium FAPI, inayotoa matibabu ya kulenga moja kwa moja kwa saratani zilizo katika hatua za juu.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wa Iran wamepiga hatua kubwa katika nyanja ya teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani licha ya vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi.
Hii ni mara ya 18 kwa Iran kuadhimisha siku ya kitaifa kuonesha mafanikio yake katika sekta ya nyuklia.

Wakati huo huo Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami, amesisitiza uwezo wa ndani wa Iran katika sayansi ya nyuklia, akieleza kuwa mataifa ya Magharibi yameshindwa kuinyima Jamhuri ya Kiislamu teknolojia hiyo.
Akizungumza wakati wa sala ya Ijumaa jijini Tehran, Eslami ameeleza kuwa nchi za Magharibi zinataka kuhodhi teknolojia ya nyuklia kwa kutumia upendeleo na vikwazo vya kisiasa, huku zikikataa kustahimili maendeleo ya programu ya nyuklia ya Iran.
Amesema: “Jambo muhimu ni kuwa tumevuka 'mistari myekundu' waliyojiwekea kiholela na kinyume cha sheria katika ug awa nyuklia."
Eslami ameongeza kuwa teknolojia ya nyuklia sasa si tu uwezo wa kisayansi, bali imekuwa sehemu ya urithi wa kitaifa — rasilimali ya kimkakati iliyokita mizizi kwenye fikra na dhamira ya watu wa Iran, ikiendelea kukua na kusonga mbele.
Halikdhalika amesisitiza kuwa mataifa ya Magharibi "hayawezi kukubali uwepo wa taifa huru kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, linalosimama sambamba nao katika majukwaa ya kimataifa."
Eslami aidha amebaini kuwa juhudi zote za mataifa ya Magharibi za kuzuia maendeleo ya Iran zimegonga mwamba. Amesema: “Kwa rehema za Mwenyezi Mungu, hawajapata mafanikio yoyote kupitia hujuma au upinzani wao, na hawatfanikiwa kamwe."
Katika muktadha wa kiteknolojia, Eslami amesema kuwa zaidi ya mataifa 30 duniani yanaonesha nia ya kununua bidhaa za nyuklia kutoka Iran , hii ikiwa ni ishara ya uhalisia wa uwezo wa teknolojia ya nyuklia nchini.
Aidha, amekosoa vikali nafasi ya Marekani katika kuzuwia Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuhimiza matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia duniani.
Amefichua kuwa: “Iran ndiyo nchi iliyopitia idadi kubwa zaidi ya ukaguzi wa IAEA kuliko nchi nyingine yoyote."
Licha ya hali hiyo, bado kuna madai kutoka kwa mataifa ya Magharibi kwamba Iran haikubali ufuatiliaji na inaendeleza shughuli za nyuklia kwa siri , madai ambayo Eslami aliyapuuza kama propaganda isiyo na msingi.
Katika miaka ya karibuni, kila mara Iran ilipokaribia kufikia makubaliano ya ujenzi wa mitambo ya nyuklia na mataifa ya kigeni, mashinikizo kutoka kwa Magharibi yamewalazimu wawekezaji kujiondoa kwenye miradi hiyo. Amehitimisha kwa kusema: "Pamoja na vikwazo vya Marekani na vizuizi vya Magharibi, tumefanikisha mafanikio makubwa katika programu yetu ya nishati ya nyuklia ya amani."

Viwango vya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga barani Afrika vimepungua tangu mwaka 2000, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebaini katika ripoti mpya.
Kati ya mwaka 2000 na 2020, vifo vya akina mama katika ukanda wa Afrika vilipungua kwa asilimia 40, kutoka vifo 727 hadi 442 kwa kila vizazi hai 100,000, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kasi ya kupungua kwa vifo hivyo bado haitoshi kufikia lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) la kuwa na vifo chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 60 ya nchi za Afrika sasa zinaripoti kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto huzaliwa kwa msaada wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, ongezeko kutoka asilimia 28 mwaka 2010. Lakini pamoja mafanikio haya, bado kuna mapengo makubwa hasa katika maeneo ya vijijini na yale yaliyoathiriwa na migogoro.
WHO ilisisitiza kuwa: “Vikwazo vikuu vya maendeleo ni pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha, udhaifu katika utawala, uhaba wa wafanyakazi wa afya, na misukosuko ya mara kwa mara kama vile milipuko ya magonjwa na migogoro – yote ambayo huvuruga huduma za afya ya mama na mtoto. Katika maeneo dhaifu na yaliyoathirika na migogoro, wanawake na watoto wako kwenye hatari zaidi.”
Ukanda huu bado unachangia asilimia 70 ya vifo vinavyohusiana na ujauzito na kujifungua duniani, huku kukikadiriwa vifo vya akina mama 178,000 na vifo vya watoto wachanga milioni moja kila mwaka barani Afrika.
Shirika hilo limebainisha sababu kadhaa zinazochangia vifo vya akina mama, ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi, maambukizi, shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito, matatizo wakati wa kujifungua, na utoaji mimba usio salama. Vifo vya watoto wachanga kwa kawaida husababishwa na kuzaliwa kabla ya wakati, matatizo ya kujifungua, na maambukizi. Vifo hivi vingi vinaweza kuzuilika iwapo hatua za haraka zitachukuliwa.
WHO imesisitiza haja ya kuongeza kasi ya juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto mchanga barani Afrika.
Dkt. Chikwe Ihekweazu, Kaimu Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema: “Katika maeneo mengi, ujauzito na kujifungua bado ni matukio ya kuhatarisha maisha ... Kila dola inayowekezwa katika afya ya mama na mtoto inaleta faida kubwa: familia zenye afya, jamii imara na ukuaji wa uchumi endelevu."