Jan 06, 2025 07:04 UTC
  • Taasisi ya Chanjo ya Razi ya Iran yaadhimisha miaka 100  tangu kuanzishwa

Karibuni kujiunga nami katika Makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu nchini Iran katika uga wa Sayansi, Tiba na Teknolojia.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ametuma ujumbe wa pongezi kwa munasaba wa kuwadia miaka 100 ya kuanzishwa taasisi ya Chanjo ya Razi. Amesisitiza kwamba taasisi hiyo, kama kituo cha kisayansi cha kutegemewa, imekuwa na jukumu muhimu katika kutengeneza chanjo zinazohitajika nchini.

Rais wa Iran alitoa matamshi hayo katika ujumbe kwa hafla iliyofanyika kwa heshima hiyo mjini Tehran Januari 5.

Amesema uzalishaji wa chanjo mbalimbali kwa mifugo na ndege wa kufugwa, chanjo saba kutoka kwenye orodha ya chanjo za binadamu, na maendeleo ya chanjo ya kwanza ya sindano-na kuvuta pumzi ya Covid-19 duniani ni sehemu tu ya huduma za thamani za taasisi hiyo, ambayo ni chanzo cha fahari kwa kila Muirani.

Taasisi ya Utafiti wa Chanjo na Seramu ya Razi ina aina mbalimbali za bidhaa za dawa zinazoweza kuendeleza uchumi wa afya na kusababisha maendeleo zaidi ya mauzo ya nje yasiyotegemea mafuta kwa kuuza bidhaa mbalimbali za kibayolojia kwa nchi za kanda. Hivi karibuni imeanzisha kituo cha utafiti na maendeleo kwa kizazi kipya cha chanjo za recombinant.

Zaidi ya hayo, watafiti na maprofesa wenye motisha na bidii wamechangia katika kuunda jukwaa ambapo malengo haya yanaweza kutekelezwa.

Taasisi ya Utafiti wa Chanjo na Seramu ya Razi ilianzishwa tarehe 6 Januari 1925, kwa kukabiliana na janga la Rinderpest. Taasisi ya Razi imekuwa mstari wa mbele katika uzalishaji wa chanjo na seramu nchini Iran. Leo, inatoa orodha tofauti ya zaidi ya bidhaa 80 za kibayolojia, ikionyesha miaka mingi ya utafiti wa kujitolea na uvumbuzi wa wanasayansi wake.

Taasisi ya Utafiti wa Chanjo na Seramu ya Razi ina matawi sita kote Iran—katika Mashhad, Ahvaz, Shiraz, Kerman, Marand, na Arak—ikihakikisha kuwa mahitaji ya uzalishaji wa chanjo na utafiti wa ndani yanatimizwa, huku kituo chake kikuu kikiwa Karaj.

Wakati taasisi hiyo inapoadhimisha hatua hii muhimu, inatafakari karne ya huduma kwa afya ya umma na inatarajia maendeleo zaidi katika uendelezaji wa chanjo.

Wakati wa janga la Covid-19, Razi Cov Pars, chanjo ya pili iliyotengenezwa na Iran dhidi ya virusi vya corona, ilitengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Chanjo na Seramu ya Razi.

@@@

Mkutano wa kimataifa kuhusu akili mnemba kwa Kiingereza Arfiticial Intelligence (AI) katika sekta ya afya ulifanyika kuanzia Januari 1 hadi 5 katika Kituo cha Mikutano cha Razi katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Kwa sasa, akili mnemba ina jukumu muhimu katika kuzuia na kugundua magonjwa mapema, pamoja na kukuza matibabu ya kibinafsi kwa kuchambua data na kulinganisha matokeo.

Takwimu zimeonyesha kupungua kwa gharama za matibabu kwa kiwango kikubwa, takriban asilimia 40, kupitia matumizi ya akili mnemba katika sekta ya afya katika nchi zilizoendelea.

Mostafa Qaemi, katibu wa Makao Makuu ya Maendeleo ya Biolojia, amesema katika baadhi ya kesi maalum, kama vile saratani ya matiti au mapafu, akili mnemba inaweza kupunguza gharama za huduma za afya kwa asilimia 80, hivyo basi uchumi wa maarifa au knowledge based economy unapaswa kulenga kutumia AI ili kuokoa gharama za afya.

Amesema kwa sasa, kampuni 17 za ndani ya Iran zinatumia akili mnemba katika uzalishaji wao wa kiteknolojia..

Wakati huo huo Chuo Kikuu Mahiri cha Sayansi za Tiba cha Iran (Smart University of Medical Sciences -SMUMS-) kimeandaa hati ya afya mahiri, ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho za kuidhinishwa.

Daktari Hassan Bakhtiari, rais wa chuo hicho amesema hati hiyo, pindi itakapopitishwa, itakuwa hatua muhimu kuelekea mabadiliko ya kidijitali katika mfumo wa afya wa nchi, tovuti ya wizara ya afya ilinukuu.

Aliyasema haya katika mkutano uliofanyika kabla ya ufunguzi wa kongamano la pili la kimataifa kuhusu akili mnemba (AI) katika sayansi za tiba lililofanyika Tehran kuanzia Desemba 18 hadi 20.

Amesema Kituo cha utafiti cha Chuo Kikuu Mahiri cha Sayansi za Tiba cha Iran ni mahali panapofaa kwa ajili ya kufanya tafiti za kivitendo na kuajiri watafiti wa matibabu. Kituo hicho pia kinaweza kusaidia kukuza matibabu na kupunguza gharama za matibabu.

Akisisitiza kuwa nchi nyingi za kanda ni vinara katika matumizi ya akili mnemba, alisema: "Iran inahitaji kuimarisha nafasi yake katika sekta ya akili mnemba katika eneo hili."

Akili Mnemba ina jukumu muhimu katika utambuzi, kinga, na matibabu ya magonjwa. Pia huboresha ubora wa huduma za matibabu.

Daktari Bakhtiari aliendelea kusema kuwa kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba, upanuzi wa huduma za matibabu katika maeneo yaliyo na changamoto za upatikanaji na vijijini unaweza kuwekwa kwenye ajenda.

Aliongeza kuwa huduma za tiba mtandao (Telemedicine) ni mojawapo ya maeneo ambayo Akili Mnemba inaweza kusaidia kuanzisha usawa wa huduma za afya kwa kutoa upatikanaji wa huduma za matibabu za hali ya juu katika maeneo ya mbali.

Kongamano la pili la kimataifa kuhusu Akili Mnemba katika sayansi za tiba limeandaliwa na Chuo Kikuu Mahiri cha Sayansi za Tiba. Limejikita katika mada kama vile afya dijitali, uchakataji wa data za matibabu, tiba za kibinafsi, na matumizi ya akili mnemba katika sekta za madawa na vifaa vya matibabu.

@@@

Na Kulingana na Mtihani wa Kimataifa wa uwezo wa akili au IQ, uliosasishwa Januari 1, Iran inashika nafasi ya pili duniani, ikiwa na wastani wa uwezo wa Akili (IQ) wa 106.63.

IQ ni kipimo cha uwezo akili kilichoundwa kuainisha watu katika makundi mbalimbali. Katika uainishaji huu, asilimia 98 ya watu hupata alama kati ya 70 na 130, na asilimia 50 hupata alama kati ya 90 na 110. Kadri alama ya IQ inavyozidi kutoka wastani wa 100, ndivyo idadi ya watu wenye alama hiyo inavyopungua. Ni asilimia 2 pekee ya watu wanaopata alama chini ya 70 au zaidi ya 130.

Matokeo ya sasa yanatokana na watu 1,393,066 duniani kote walioufanya mtihani huo kwenye tovuti husika mwaka wa 2024.

China na Korea Kusini zinashika nafasi ya kwanza na ya tatu, zikiwa na wastani wa IQ wa 107.43 na 106.57 mtawalia.

Wastani wa IQ kwa nchi unaonekana kuwa wa juu zaidi katika  bara la Asia ya Mashariki. Kiwango cha IQ ni cha wastani barani Ulaya, Asia ya Magharibi, Oceania, Amerika Kaskazini na Afrika Kaskazini. Aidha IQ imetajwa kuwa chini ya wastani katika nchi Afrika ya Kati na Kusini, na Amerika ya Kusini.

Iran ni mojawapo ya nchi bora zaidi duniani katika orodha hiyo. Mafanikio haya yanaonyesha uwezo mkubwa wa kiakili wa watu wa Iran.

Mambo kama vile utamaduni, msisitizo katika sayansi za msingi, na nafasi ya familia katika kulea vipaji ni miongoni mwa sababu kuu za mafanikio haya.

Hata hivyo, matokeo haya mashuhuri yanaweza kuchochea mipango mipya ya kutumia vipaji hivi kwa maendeleo endelevu ya nchi.

Nchi zinazofuata Iran, China na Korea Kusini ni Japani (106.54), Singapore (105.25), Urusi (103.31), Mongolia (103.13), Australia (102.67), Armenia (102.64), na Uhispania (102.37) ni miongoni mwa nchi kumi bora.

Kati ya nchi kumi bora katika IQ, sita zinatoka Asia, jambo linaloonyesha ubora wa eneo hilo katika maendeleo ya binadamu.

Nchi za Asia, hasa Asia Mashariki na Kusini-Mashariki, zina mafanikio makubwa katika uwanja wa akili za jumla kutokana na msisitizo wao katika elimu madhubuti na matumizi ya teknolojia mpya katika kujifunza.

Kipimco cha Kimataifa cha IQ kinategemea mbinu za Raven (zilizoanzishwa na mwanasaikolojia John Carlyle Raven mnamo 1936). Kwa kila swali, mhusika lazima ajibu kwa kutumia mantiki. Mbinu hii hupima uwezo wa kufikiri na kuelewa mambo magumu.