Nov 30, 2023 14:51 UTC
  • Iran yaongoza katika uwanja wa matibabu ya macho Asia Magharibi

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika. @@@


Iran inashika nafasi ya kwanza katika uwanja wa matibabu ya macho au opthalmolojia kati ya nchi za Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na inashindana na nchi zilizoendelea zaidi duniani katika suala hili.

Mwenyekiti wa Idara ya Opthalmolojia katika Wizara ya Afya ya Iran, Dk Mahmoud Jabbarvand, amesema Iran imekuwa ikikaribisha mamilioni ya watalii wa matibabu kila mwaka na kwamba hakuna mgonjwa wa Iran anayetumwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Jabbarvand amesema hivi karibuni kwamba, kwa kuzingatia upeo wa utafiti na tafiti katika uwanja wa magonjwa ya macho, Iran inaweza kulinganishwa na nchi zilizoendelea duniani.

Aliongeza: "Kwa sababu ya wingi wa huduma za matibabu ya macho hapa Iran, hakuna mgonjwa anayepelekwa nje ya nchi na hata wagonjwa wengi kutoka nchi tofauti, hasa jirani, hufunga safari na kuja Iran kupata  matibabu."

Aidha alisema Iran imepata utaalamu wa kutengeneza  konea na kuongeza kuwa upandikizaji wa konea hufanywa kwa wagonjwa ambao hawawezi kupokea tishu za binadamu wala seli shina.

Jabbarvand alisema wale ambao wamefanyiwa upasuaji huo wameweza kurejesha uwezo wao wa kuona vizuri,.

Alifafanua kuwa madaktari wa macho wapatao 2,500 hivi sasa wanafanya kazi nchini Iran, ambayo imepata maendeleo makubwa katika uwanja wa uwekaji wa seli za shina.

Halikadhalika wataalamu wa Iran wanaweza kufanya utafiti kwa ustadi wa kina.

Afisa huyo mwandamizi wa afya nchini Iran  alisema:"Kwa sababu ya utaalam mkubwa na utendaji mzuri wa madaktari wetu, pamoja na uendeshaji mzuri wa hospitali za serikali na za kibinafsi, wagonjwa ambao wanagunduliwa kwa wakati hufanyiwa upasuaji haraka na kupata tena uwezo wao wa kuona."

Wanasayansi wa Iran wameendelea kuwa na mafanikio katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na kuwepo vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimefanya iwe vigumu kwa vyuo vikuu kununua baadhi ya vifaa vya juu zaidi au kutuma wanafunzi wenye vipaji Ulaya au Marekani kuhudhuria mikutano ya kisayansi.

Tehran, Mashhad, Yazd, Shiraz na Ahvaz ni miongoni mwa maeneo yaliyochaguliwa na watalii wa matibabu, ambao huchagua kuvuka mipaka kutafuta matibabu ya bei nafuu nchini Iran.

@@@

Mradi wa kwanza wa mfumo wa satelaiti nchini Iran uliopewa jina la kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani utawekwa kwenye anga za juu yaani obiti ndani ya miaka miwili ijayo.

Hayo ni  kwa mujibu wa Hossein Salariyeh mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran (ISA) ambaye ameongeza kwamba shirika, sambamba na juhudi za kutoa huduma za vituo vya anga za juu katika nyanja ya mawasiliano hususani Teknolojia ya Intaneti katika Vitu  yaani Internet of Things kwa kifupi, IoT, pia limetayarisha maelezo ya kiufundi ya satelaiti ya kwanza ya mawasiliano ya mkondo mwembamba ya asili na kukaribisha kampuni zinazohusika na maarifa. kuchangia sehemu yao kwenye mradi.

Afisa huyo mkuu wa anga za juu nchini Iran  alisema kwamba mradi wa mfumo wa satelaiti unajengwa hatua kwa hatua, na utawekwa kwenye obiti ndani ya miaka miwili ijayo kwani satelaiti kadhaa zilizotengenezwa nchini tayari zinasubiri kurushwa angani.

Salariyeh alisema: "Satelaiti ya Shahidi Soleimani itatoa huduma za Intaneti katika Vitu  (IoT) ambapo itakusanya data kutoka ardhini na kuisambaza kwa kituo cha marejeleo. Mungu akipenda, idadi na uwezo wa satelaiti zinazohusika zitaongezeka baadaye,”

Mkuu huyo wa ISA alibainisha kuwa Mfumo wa Satelaiti ya Shahidi Soleimani Utajumuisha satelaiti kadhaa ambazo zitawekwa katika obiti ya chini ya sayari ya Dunia (LEO), akiusifu mradi huo kama wa kwanza wa aina yake nchini Iran na hata ulimwengu wa Kiislamu.

Mfumo huo umetengenezwa na wataalamu wa Iran kikamilifu na kwa sasa unaendelea kujengwa.

Licha ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeweza kupiga hatua kubwa katika mpango wa anga ya juu wa kiraia.

Nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 10 bora duniani zenye uwezo wa kutengeneza na kurusha satelaiti.

@@@@

RAIS William Ruto wa Kenya  hivi karibuni amezindua simu ya mkononi ya bei nafuu itakayowasaidia Wakenya kupata huduma za serikali mitandaoni.

Simu hizo ambazo zimetengenezwa na kampuni ya East Africa Device Assembly Kenya (EADAK) Ltd iliyoko eneo la Mavoko, Kaunti ya Machakos, itauzwa kwa bei ya rejareja ya Shilingi za Kenya 7,499 au takribani dola 50.

Zitauzwa katika maduka ya Faiba, maduka ya Safaricom na maduka mengine ambayo huuza simu kote nchini.

Simu hizo chapa Neon 5 ‘Smarta’ na 6 ½ ‘Ultra’  zitakuwa na uwezo wa kutumia mawimbi ya 4G.

Kiwanda hicho cha Mavoko kilianzishwa kupitia ushirikiano kati ya kampuni za simu za humu nchini na kampuni za kutengeneza simu katika mataifa ya ng’ambo.

Mwenyekiti wa EADAK Joshua Chepkwony alisema: “Kiwanda hicho kitapiga jeki ajenda ya serikali ya kuendeleza shughuli za kidijitali nchini kando na kuzalishaji nafasi nyingi za ajira moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja.”

@@@

Na takribani kifo 1 kati ya 3 hutokana na saratani ya ngozi isiyoanzia kwenye seli ya mwili wa binadamu au Non-Melanoma na husababishwa na kufanyia kazi juani.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya makadirio mapya ya Umoja wa Mataifa lile la afya WHO na lila la kazi ILO yamesema.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa Geneva Uswisi na WHO imeeleza kwamba utafiti uliochapishwa katika jarida la Environment International unaonesha kuwa wafanyakazi wa nje ndio wanaothirika vibaya na aina hiyo saratani ngozi na hivyo wametoa wito wa kuchukua hatua za haraka kuzuia hatari hii mahali pa kazini na upotevu wa maisha ya wafanyakazi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhenom Ghebreyesus amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema mionzi ya jua bila kinga ni sababu kubwa ya saratani ya ngozi pahala pa kazi na kuongeza kwamba “kuna suluhisho madhubuti za kulinda wafanyakazi dhidi ya miale hatari ya jua na kuzuia athari zake zenye madhara".

Kulingana na makadirio hayo, mwaka 2019 watu bilioni 1.6 wenye umri wa kufanya kazi (yaani kuanzia miaka 15 au zaidi) walikumbwa na mionzi ya jua wakati wakifanyia kazi nje sawa na 28% ya watu wote wenye umri huo kwa mwaka huo pekee, huku takribani watu 19,000 katika nchi 183 walifariki kutokana na saratani hiyo ya ngozi kwa sababu ya kufanya kazi nje kwenye jua. Asilimia 65 walikuwa wanaume.

Makadirio hayo yanathibitisha kwamba mionzi ya jua kazini kama chanzo cha tatu hatari kinacholeta mzigo mkubwa wa vifo vya saratani duniani kote.

Kutokana na utafiti huo, WHO inataka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwalinda wafanyakazi kutokana na hatari ya kufanya kazi kwenye jua, na kusisitiza wafanyakazi lazima walindwe dhidi ya mionzi ya jua kazini tangu wakiwa na umri wa kufanya kazi.

WHO, ILO, Shirika la Hali ya Hewa Duniani na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa wamezindua hivi karibuni programu ya SunSmart Global UV App ambayo wafanyakazi wa nje wanaweza kutumia kupima kiasi cha kukukumbwa na mionzi ya ultraviolet ya jua.

Pia, hatua za kupunguza hatari ya saratani ya ngozi ni pamoja na kuongeza ufahamu wa wafanyakazi wakati kufunuliwa kazini kwa mionzi ya ultraviolet ya jua na jinsi inavyosababisha saratani ya ngozi, na kutoa huduma na mipango ya kugundua dalili za awali za saratani ya ngozi.

 

Tags