Jul 01, 2024 05:50 UTC
  • Tume: Watu milioni 9.7 wametimiza masharti ya kupiga kura nchini Rwanda

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Rwanda imetoa orodha ya mwisho ya wapiga kura, ikionyesha kwamba watu milioni 9.7 wametimiza masharti ya kushiriki katika uchaguzi wa mwezi huu wa Julai wa kuchagua rais na wabunge katika wilaya 30 za Rwanda na Wanyarwanda wanaoishi nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo idadi yote ya wananchi wa Rwanda ni milioni 13. Orodha hiyo ya mwisho imetolewa Jumamosi baada ya kusasishwa daftari la wapiga kura na baadaye kufungwa.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Rwanda, Oda Gasinzigwa alitangaza habari hiyo jana Jumapili kupitia televisheni ya taifa na kuongeza kuwa: "Wanyarwanda wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wamo kwenye daftari la wapiga kura. Kila mpiga kura atatakiwa kuonesha kitambulisho cha taifa ili waruhusiwe kupiga kura tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, kadi ya kupigia kura tu ndiyo iliyokuwa inatumika."

Kampeni za uchaguzi nchini Rwanda

 

Tume hiyo pia imetangaza kuwa vituo 2,591 vya kupigia kura vimetengwa ili kuwezesha uchaguzi huru wa haki. Uchaguzi huo utafanyika kwa muda wa siku tatu kati ya Julai 14 hadi Julai 16.

Raia wa Rwanda walioko nje ya nchi watapiga kura zao za rais na wabunge tarehe 14 Julai katika balozi za nchi hiyo huku wapiga kura ndani ya Rwanda wataanza kupiga kura tarehe 15 Julai. 

Baada ya kupitishwa mchujo na bodi ya uchaguzi ya Rwanda, hivi sasa wamebakishwa wagombea watatu katika kinyang’anyiro cha urais, akiwemo Rais wa hivi sasa Paul Kagame, Frank Habineza wa chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda na Philippe Mpayimana, mgombea binafsi. Waliobakishwa katika kinyang'anyiro cha viti 80 vya bunge ni wagombea 500.