Jul 03, 2024 02:50 UTC
  • Ripota wa UN aipongeza Uhispania kwa kujiunga na kesi ya mauaji ya halaiki ya Afrika Kusini dhidi ya Israel

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ameipongeza Uhispania kwa kuunga mkono kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inayoituhumu Israel kuwa imefanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.

Katika ujumbe wake  kwenye mtandao wa X, Francesca Albanese alikaribisha uamuzi wa Uhispania wa kujiunga na kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kuhusu vita vyake dhidi ya watu wa Gaza, ambako imeua karibu Wapalestina elfu 40 tangu Oktoba 7, mwaka jana.

Albanese alisema anatumai hatua ya Uhispania ni mwanzo wa hatua kama hiyo za nchi nyingine za Magharibi ya "kusimama upande sahihi wa historia."

“Matamshi ya kulaani bila vitendo hayana maana. Miongo kadhaa ya maneno matupu imeiruhusu Israel kupanua ukiukaji wake wa sheria dhidi ya Wapalestina hadi kutenda mauaji ya kimbari," ameandika Francesca Albanese.

Amesisitiza kuwa nchi za Magharibi hazijachelewa sana kujiunga na upande wahihi wa historia. 

Katika upande mwingine, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa  ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati ya kukamatwa "mpangaji" wa sera za mauaji ya kimbari ya Israeli, Bezalel Smotrich.

Bezalel Smotrich

Akiwasilisha ripoti yake iliyopewa jina la "Anatomy of a Genocide" katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Albanese amesema, "Kuvuliwa sifa ya binadamu kwa Wapalestina kama kaumu ni kielelezo kikuu cha historia yao - inayoambata na maangamizii ya kizazi, kupokonywa ardhi na ubaguzi wa rangi, (apartheid)."

Katika ripoti hiyo, Albanese alisema kuwa Israel imefanya nauaji ya kimbari yaliyopigwa marufuku katika Mkataba wa Geneva, ikiwa ni pamoja na kuua raia wa Palestina.