Sunak ainua mikono juu, akiri kushindwa vibaya Chama cha Conservative, Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i113712-sunak_ainua_mikono_juu_akiri_kushindwa_vibaya_chama_cha_conservative_uingereza
Waziri Mkuu wa Uingereza na kiongozi wa Chama cha Conservative, Rishi Sunak, amekiri kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika jana, Alhamisi.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 05, 2024 03:59 UTC
  • Rishi Sunak
    Rishi Sunak

Waziri Mkuu wa Uingereza na kiongozi wa Chama cha Conservative, Rishi Sunak, amekiri kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika jana, Alhamisi.

Sunak - ambaye amehifadhi kiti chake cha ubunge huko Richmond kaskazini mwa Uingereza - amesema kuwa amempigia simu mpinzani wake, Keir Starmer, kiongozi wa Chama cha Labour, ili kumpongeza kwa ushindi wa chama chake katika uchaguzi huo.

Awongeza kuwa: "Wapiga kura wamefanya uamuzi halisi, na kuna mengi ya kujifunza na kufikiria," akisisitiza kwamba anawajibika kikamilifu kwa kushindwa kwa chama chake.

Chama cha Labour cha Uingereza kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika jana Alhamisi, na kuhitimisha miaka 14 ya utawala wa Conservative, na hivyo kumfungulia milango kiongozi wake, Keir Starmer katika Downing Street.

Kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer 

Kulingana na matokeo ya uchaguzi huo yaliyochapishwa na televisheni ya Uingereza, chama cha Labour (katikati-kushoto) kitapata viti 410 kati ya 650 vya Bunge, kikiwatimulia kivumbi Wahafidhina, ambao watapata viti 131. Matokeo hayo ya viti vya chama tawala cha Conservative ndiyo mabaya zaidi tangu mwanzo wa karne ya 20.

Badhi ya wachambulizi wa mambo wanasema, wapiga kura wa Uingereza wamekiadhibu chama tawala cha Conservative kutokana na mgogoro wa gharama ya juu ya maisha, na siasa zake za masuala ya kigeni ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kibubusa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.