Jun 29, 2024 06:55 UTC
  • Uholanzi yafunguliwa mashtaka kwa kuipatia Israel vipuri vya ndege za kivita za F-35

Mashirika matatu ya kutetea haki za binadamu yasiyo ya kiserikali yamefungua kesi dhidi ya serikali ya Uholanzi, yakidai kwamba imekiuka marufuku ya kuipatia Israel vipuri vya ndege za kivita aina ya F-35 iliyotolewa Februari mwaka huu.

Oxfam Novib, mojawapo ya mashirika matatu yaliyofungua mashtaka hayo limesema kuwa: "Kwa bahati mbaya, kila kitu kinaonyesha kwamba vipuri hivyo vinavyotoka Uholanzi vinafika Israel kupitia njia za mzunguko."

Serikali ya Uholanzi "imeendelea kupeleka vipuri vya ndege za F-35 kwa nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Marekani. Hii inapingana na uamuzi wa mahakama," Lisbeth Ziegveld, wakili anayewakilisha NGOs tatu, ameiambia mahakama ya Uholanzi.

Ameongeza kuwa: "Uamuzi wa mahakama unahusu vipuri vyote vya ndege ya F-35 ambavyo mwisho wake ni Israel, na serikali lazima isitishe usafirishaji wote kama huo."

Katika uamuzi wa kihistoria uliotolewa Februari mwaka huu, Mahakama ya Rufaa ya Uholanzi iliiamuru serikali ya nchi hiyo kuacha kuipatia Israel vipuri vya ndege hizo zinazotumiwa kuua raia katika Ukanda wa Gaza.

Gaza

Hadi sasa Israel imeua karibu Wapalestina elfu 40 wa Ukanda wa Gaza wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo.