Jul 01, 2024 10:26 UTC
  • Jeshi la Sudan lakomboa Sinja, mapigano yalazimisha watu 55,000 kukimbia

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limefanikiwa kudhibiti wa makao makuu ya kitengo cha 17 cha jeshi la nchi kavu, makao makuu ya Brigedia ya 67, na vitongoji vyote vya kusini na mashariki vya mji wa Sinja, makao makuu ya Jimbo la Sennar kusini-mashariki mwa Sudan.

Ripoti zinasema jeshi la Sudan limethibitisha kuwa kundi la Rapid Support Forces limepoteza mamia ya wapiganaji wake katika mapigano hayo yanayoendelea tangu Jumamosi iliyopita.

Awali, msemaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), Al-Fatih Qureshi, alisema kuwa wapiganaji wa kundi hilo walidhibiti kikamilifu mji wa Sinja siku ya Jumamosi na makao makuu ya Kitengo cha 17 cha jeshi la Sudan.

Qureshi alisema - katika taarifa hiyo - kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka pia vimeteka magari 112 ya kijeshi na mizinga 6.

Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa zaidi ya watu 55,000 wamekimbia makazi yao katika mji wa Sinja na vijiji vya kandokando yake, wakikimbia vita vikali kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka.

Taarifa ya IOM imeongeza kuwa "hali bado ni ya wasiwasi na haitabiriki."

Kwa upande wake, Kituo cha Kuchunguza Haki za Binadamu cha Al-Sinari (kikundi cha kujitolea) kimesema kuwa Kikosi cha Msaada wa Haraka kinawashikilia makumi ya wagonjwa wa kiraia na wafanyikazi wa matibabu kama ngao za binadamu ndani ya Hospitali ya Mafunzo ya Sinja.