Jun 30, 2024 06:57 UTC
  • Wagombea 2 wa urais Iran kushiriki katika midahalo miwili

Wagombea wawili wa kiti cha rais nchini Iran, Masoud Pezeshkian na Saeed Jalili wanatazamiwa kushiriki midahalo miwili ya urais kabla ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Shirika la habari la Mehr limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mdahalo wa kwanza wa wagombea hao utafanyika kesho Jumatatu mwendo wa saa 3:30 usiku kwa saa za hapa Iran, huku wa pili ukitazamiwa kufanyika Jumanne usiku.

Matokeo rasmi ya duru ya 14 ya uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wa Iran yanaonesha kuwa zoezi hilo litaingia katika duru ya pili iliyopangwa kufanyika Julai 5, ikiwachuanisha Masoud Pezeshkian ambaye amewahi kuwa Waziri wa Afya na mbunge wa sasa, na mkuu wa zamani wa timu ya mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili. 

Mohsen Eslami, Msemaji wa Makao Makuu wa Uchaguzi ya Iran amesema baada ya kuhesabiwa kura zote zilizopigwa (24,535,185) kwenye uchaguzi huo wa Ijumaa ya Juni 28, Pezeshkian ameibuka kidede kwa kupata kura 10,415,991 huku Jalili akiambulia kura 9,473,298.

Wagombea wa kiti cha rais nchini Iran, Masoud Pezeshkian (kushoto) na Saeed Jalili

Wagombea wengine wawili, Spika wa Bunge, Mohammad Baqer Qalibaf na waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Mostafa Pourmohammadi, wameshika nafasi ya tatu na nne, kwa kura 3,383,340 na 206,397 kwa utaratibu huo.

Tayari Qalibaf ambaye amewahi pia kuwa Meya wa jiji la Tehran amewaasa wafuasi wake wampigie kura Jalili katika duru ya pili ya uchaguzi huo itakayofanyika Ijumaa ijayo. Wagombea hao wanne walichuana kuwania kiti cha Urais kilichobakia wazi baada ya kufariki dunia aliyekuwa Rais wa Iran, Shahidi Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta, tarehe 19 Mei mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Kaimu Rais wa Iran, Mohammad Mokhber amewapongeza wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo. Amesema, ushiriki huo wa mamilioni ya Wairani kwenye zoezi hilo ni dhihirisho jingine la demokrasia ya kidini.

 

 

Tags