Jun 28, 2024 09:17 UTC
  • Ramaphosa aomboleza mauaji ya wanajeshi wa A/Kusini DRC

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameelezea kusikitisha mno na mauaji ya wanajeshi wawili wa nchi yake na kujeruhiwa wengine 20 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wanajeshi hao ni kutoka Kikosi cha Ulinzi wa Taifa cha Afrika Kusini (SANDF) na walishambuliwa kwa roketi wakiwa kwenye moja ya kambi zao katika mji wa Sake, mashariki mwa DRC siku ya Jumanne.

Taarifa ya Ikulu ya Rais wa Afrika Kusini imesema kuwa, Ramaphosa ametoa mkono wa "rambi rambi" kwa familia za wanajeshi waliouwa na waliojeruhiwa pamoja na makamanda wao na wanajeshi wenzao.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema, Rais Ramaphosa anawaombea dua pia askari wa SANDF waliojeruhiwa ili waweze kupata nafuu ya haraka kutokana na majeraha yao,

Vile vile rais huyo wa Afrika Kusini amezihakikishia familia zilizofiwa na wanajeshi waliojeruhiwa kwamba SANDF itaziangalia kwa uangalifu wa hali ya juu na kutoa msaada unaohitajika wa vifaa na kisaikolojia kwa wale wote walioathiriwa.

Amesema: Wakati huu tunapowaomboleza askari wetu waliouawa na waliojeruhiwa (huko DRC), tunathamini na tuheshimu mno kujitolea kwao kwa ajili ya kuleta amani na utulivu ndani na nje ya Afrika Kuisni na hawatasahaulika.

Wanajeshi hao wa Afrika Kusini ni sehemu ya Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC waliokuwa wanahudumu huko DRC. Askari hao walipelekwa huko mwezi Disemba 2023 ili kusaidia juhudi za serikali ya DRC za kurejesha amani na usalama mashariki mwa nchi hiyo.