Jun 30, 2024 11:25 UTC
  • Watu 18 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi jimboni Borno, Nigeria

Kwa akali watu 18 wamepoteza maisha huku makumi ya wengine wakijeruhiwa kufuatia wimbi la mashambulizi ya kigaidi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Barkindo Saidu, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Dharura katika jimbo hilo amesema magaidi wanawake waliokuwa wamejifunga mabomu walijiripua kwenye mikusanyiko ya watu waliokuwa harusini, kwenye mazishi na hospitalini, na kusababisha vifo hivyo.

Ameongeza kuwa, mbali na watu 18 kuthibitishwa kuuawa katika hujuma hizo mjini Gwoza, wakiwemo watoto na wanawake wajawazito, wengine zaidi ya 30 wamejeruhiwa.

Polisi ya Nigeria haijatoa taarifa kuhusiana na mashambulio hayo ya kigaidi ya jana Jumamosi. Aidha hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hizo, ingawaje magenge ya kigaidi ya Boko Haram na ISIS tawi la Afrika Magharibi (ISWAP) yamekuwa yakifanya hujuma za aina hii.

Wanachama wa kundi la kigaidi la ISWAP

Nigeria katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na mashambulizi ya magenge ya uhalifu yakiwemo makundi ya magaidi wa Boko Haram na ISWAP katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo, hasa ya kaskazini. 

Umwagaji damu huu unaendelea Nigeria katika hali ambayo, jeshi la nchi hiyo hivi karibuni lilisema kuwa limewaangamiza magaidi 2,245 katika oparesheni dhidi ya wanamgambo wa kitakfiri wa Boko Haram na ISWAP katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. 

Tags