Jumatano, Oktoba Mosi, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiul-Thani 1447 Hijria Qamaria, sawa na tarehe 9 Mehr mwaka 1404 Hijria Shamsia, inayosadifiana na tarehe Mosi Oktoba 2025 Miladia.
Miaka 2347 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Mosi Oktoba mwaka 322 BC, aliaga dunia mwanafalsafa mashuhuri wa Ugiriki ya kale, Aristotle akiwa na umri wa miaka 62. Aristotle alizaliwa mwaka 384 BC katika mji wa Stagira ambao leo hii ni sehemu ya jimbo la Ugiriki la Macedonia ya Kati. Baba yake alikuwa daktari wa mfalme wa Macedonia, na kwa sababu hiyo alirithi mali nyingi kwa baba yake ambaye aliaga dunia, yeye akiwa angali kijana mdogo. (Kwa mtazamo wa mwanafalsafa huyo wa Kigiriki, maisha ya fanaka hupatikana kwa kuwa na uvumilivu, sambamba na kuzingatia msingi wa kiasi na wastani katika ufanyaji mambo; na maisha ya furaha nayo hupatikana kwa kuishi vizuri unakotokana na kufanya kazi vizuri.)

Katika siku kama ya leo miaka 1214 iliyopita, yaani tarehe 8 Rabiu-Thani, mwaka 232 Hijria Qamaria alizaliwa katika mji wa Madina, Imamu Hassan al-Askari mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume SAW. Akiwa katika umri wa utotoni, alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS, kuondoka mji huo na kuhamia Samarra, Iraq ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Japokuwa mtukufu huyo hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu. (Imam Hassan al- Askari alihudumia Uimamu kwa muda wa miaka 6 tu akipitisha sehemu kubwa ya miaka hiyo michache uhamishoni na kwenye jela za Bani Abbas). Sambamba na kukupeni mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa nuru hiyo ya kizazi cha Bwana Mtume SAW nakunukulieni hapa moja ya semi adhimu za Imamu huyo mtukufu isemayo: Mwenye kuchunga zaidi haki za watu, ndiye mwenye daraja ya juu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Miaka 76 iliyopita, tarehe Mosi Oktoba 1949 ilitangazwa rasmi Jamhuri ya Watu wa China chini ya uongozi wa Mao Zedong. Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya wakoloni hasa Waingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa.

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. (Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya majeshi ya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria.) Mwaka 1914 Uingereza iliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.

Na tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani. Siku hii ilitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juuuu ndani ya familia na katika jamii.
