Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yataka kuachiliwa wanaharakati wa Sumud
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imelaani kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kuendelea kuwashikilia wanaharakati wa msafara wa kimataifa wa meli nyingi wa Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Gaza, na kutaka kuachiwa mara moja kwa raia wa Nigeria na wa mataifa mengine waliotekwa nyara na kuzuiliwa na askari wa majini wa Kizayuni.
Katika mahojiano maalum na Iran Press katika Jimbo la Bauchi, Nasir Danladi Abubakar, Mkuu wa Jukwaa la Rasilimali la Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amesema, "Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, na watu wote wa Nigeria wanaothamini ubinadamu, wanalaani vikali ukatili uliofanywa na Israel katika kuwashambulia, kuwakamata na kuwaweka kizuizini mamia ya wanaharakati wa Sumud Flotilla."
Amebainisha kuwa: Vitendo hivi vimelaaniwa na jamii ya kimataifa kwa sababu vinakiuka sheria za kimataifa. Ingawaje wanaharakati wengi wameachiliwa huru, lakini tunatoa wito kwa dunia nzima kuushinikiza utawala wa Israel kuwaachia mara moja wanaharakati waliosalia kizuizini akiwemo raia wa Nigeria, Michael Okey.
Michael Nnorom Okey, ambaye alijiunga na msafara wa Omar Al-Mukhtar uliojiunga na mfara mkubwa wa kimataifa wa Sumud, bado anazuiliwa na Israel pamoja na Wamorocco watatu, Mualgeria mmoja, na mwanaharakati mmoja wa Uhispania.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wiki liyopita alitaka pia kuachiliwa mara moja kwa Waafrika Kusini na raia wengine wa kigeni wanaozuiliwa na jeshi la Israel, baada ya wanajeshi wa majini wa utawala huo haramu kushambulia msafara wa kibinadamu uliokuwa unaelekea Gaza.
Alisema kuwa, hatua za Israel zilikiuka uhuru wa nchi ambazo bendera zao zilipeperushwa kwenye meli za msafara wa Sumud na kukiuka amri ya Mahakama ya Kimataifa inayotaka kufikishwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo huko Gaza.
Wanaharakati hao wanasisitiza kuwa, dhamira ya msafara wa Sumud ilikuwa njia moja ya kutangaza "mshikamano," na Wapalestina wa Gaza na wala sio makabiliano.