Jun 29, 2024 02:26 UTC
  • Harakati za Kiislamu za Yemen na Iraq zashirikiana tena kuupiga utawala wa Kizayuni

Wanamapambano shupavu wa harakati za Kiislamu za Iraq na Yemen kwa mara nyingine tena wameshirikiana katika operesheni ya kuyapiga maeneo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Televisheni ya al Masirah ya Yemen imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kwa kushirikiana na muqawama wa Kiislamu wa Iraq, vimeshambulia kwa makombora mji wa Haifa wa utawala wa Kizayuni, operesheni ambayo imefanyika kwa mafanikio makubwa. 

Vikosi vya Ulinzi bya Yemen vimesema katika taarifa yao kuwa, operesheni hizo za pamoja zitaendelea mpaka adui Mzayuni atakapokomesha jinai na mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza.

Wakati huo huo Hizbullah ya Lebanon nayo imetoa tamko na kusema kuwa, imepiga maeneo ya Wazayuni ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni kwa kutumia makumi ya makombora ya Katyusha.

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, operesheni hiyo imefanyika dhidi ya eneo la utawala wa Kizayuni la Biriyya, kaskazini mwa ardi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na kusababisha moto mkubwa.

Sasa hivi karibu miezi 9 tena utawala wa Kizayuni unafanya jinai kubwa dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina, jinai ambazo zinaendelea kufanyika ndani ya kimya cha kutisha cha jamii ya kimataifa na wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani.

Harakati za Kiislamu za Iraq na Lebanon pamoja na Yemen zimeamua kuingia vitani kupambana na utawala katili wa Kizayuni hadi utakapoacha kuwashambulia wananchi wa Ghaza.