Jul 01, 2024 02:22 UTC
  • Jeshi la Sudan lakanusha madai ya RSF ya kuteka makao makuu ya jimbo la Sennar

Jeshi la Sudan (SAF) jana Jumapili lilikanusha madai kwamba Askari wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wamechukua udhibiti wa mji wa Singa ambao ni makao makuu ya jimbo la Sennar la katikati mwa Sudan.

Msemaji wa Jeshi la Sudan, Nabil Abdalla, alisema katika taarifa yake kwamba: "Vikosi vyetu (vya SAF) vinaendelea kupambana na adui kwa nguvu na ari ya hali ya juu na viko imara." 

Ukanushaji huo ulitolewa jana na Jeshi la Sudan SAF baada ya madai yaliyotolewa usiku wa kuamkia jana na msemaji wa RSF, Al-Fateh Qurashi kwamba vikosi hivyo vimeudhibiti kikamilifu mji wa Singa na vinashikilia taasisi zote za mji huo pamoja na makao makuu ya serikali ya jimbo la Sennar.

Kwa upande wake, Al-Sinnari Observatory, shirika la masuala ya sheria la eneo hilo limeonya katika taarifa yake ya jana Jumapili kuhusu janga jipya la kibinadamu katika mji huo.

Sehemu moja ya taarifa ya shirika hilo imesema: "Singa imeshuhudia mapigano makali sana ya silaha na mizinga yaliyofanya uharibifu mkubwa wa mali za umma na kuwaletea madhara raia wasio na hatia.

Shirika hilo pia limesema kuwa, uchunguzi wake unaonesha kuweko maelfu ya raia waliokimbia makazi yao na kuelekea katika Jimbo la Blue Nile la kusini mwa Sudan.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya mejenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF vinaendelea kuisababishia madhara makubwa ya kila upande nchi ya Sudan huku wahanga wakuu wakiwa ni raia wa kawaida.