Jul 01, 2024 02:21 UTC
  • Nchi za Afrika zahimizwa kuharakisha utekelezaji wa AfCFTA

Nchi za Afrika zimetakiwa kuwasilisha mipango ya utekelezaji na mikakati ya kitaifa ili kuharakisha ufanikishaji wa malengo ya kuanzishwa Eneo Huria la Biashara ya Bara la Afrika (AfCFTA) na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za bara hilo.

Mwito huo umetolewa kwenye "Jukwaa la Kitaifa la Mashauriano juu ya Maendeleo ya Mkakati wa Utekelezaji wa AfCFTA wa Ethiopia" lililofanyika Addis Ababa, mji mkuu wa nchi hiyo.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Stephen Karingi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kikanda na Biashara cha Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kuhusu bara la Afrika (UNECA), amesema kuwa, iwapo maazimio AfCFTA yatatekelezwa kivitendo, yanaweza kukuza uchumi wa viwanda, uzalishaji wa ajira na uwekezaji barani Afrika.

Amesema, utekelezaji wa AfCFTA unaendelea vizuri barani Afrika na tayari kuna malengo makubwa yamewekwa kwa ajili ya kukuza biashara katika bara hilo zima.

Lakini pamoja na hayo ameelezea kusikitishwa kwake na ubovu wa miundombinu, mitandao duni ya uchukuzi na vifaa dhaifu vya mpakani. Amesema hizo bado ni changamoto ambazo zinazorotesha utekelezaji wa haraka wa mikakati ya AfCFTA.

Beyene Petros, mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sera ya Ethiopia, yeye amesema kuwa, tangu kuanza kutumika AfCFTA mwaka 2019, kumekuwa na maendeleo muhimu. Jumla ya nchi 47 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) hadi sasa zimeridhia utendaji wa AfCFTA tangu mwaka huo.

Benki ya Dunia inakadiria kuwa AfCFTA ina uwezo wa kuwatoa watu milioni 30 kwenye umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2035.