Macron aonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini Ufaransa
Katika mkesha wa uchaguzi wa mapema wa Bunge, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameonya kuhusu uwezekano wa kupata ushindi makundi ya mrengo wa kushoto na kulia yenye misimamo ya kufurutu mipaka na kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian, Macron amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Masuluhisho yanayotolewa na mrengo wenye misimamo mikali wa kulia hayawezi kujadiliwa kwa sababu yanawagawa watu kwa mujibu na dini na mbari zao, jambo ambalo linasababisha hitilafu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Tahadhari ya Rais wa Ufaransa kuhusu matokeo mabaya ya sera za udini na migawanyiko ya kimbari ni muhimu kutokana na kuwepo dini tofauti nchini Ufaransa zinazofuatwa na kaumu mbalimbali; na sera za makundi ya mirengo ya kulia na kushoto zinaweza kuyumbisha usalama na amani ya Ufaransa.
Hussein Husseini, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema kuhusu suala hili kwamba: "Ushindi wa mirengo yenye siasa kali ya kushoto na kulia nchini Ufaransa, ambao unaweza kupatikana kwa kuchochea hisia kali za utaifa, unaweza kusababisha mgawanyiko na kuimarisha mirengo yenye itikadi kali nchini Ufaransa; na matokeo yake mabaya ya kwanza ni kuchochea mivutano ya kidini na kikabila, ambayo ni hatari sana kwa usalama wa taifa wa Ufaransa." Kwa msingi huo, matamshi ya Macron yanaonyesha kuwa ameelewa hatari hizo na anajaribu kuitahadharisha jamii ya Wafaransa kuhusu sera hizo za makundi yenye kufurutu mipaka.
Tahadhari ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, imetolewa baada ya kiongozi wa chama cha National Rally (RN), Jordan Bardella kuchapisha ilani ya uchaguzi akiahidi kubana uhamiaji na kusisitiza kuwa, atafuta haki za uraia kwa watoto wanaozaliwa na kukulia nchini Ufaransa na wazazi wawili raia wa kigeni.
Akizungumza mjini Paris, Bardella alisema kipaumbele cha muda mrefu cha chama chake ni kuirejesha Ufaransa katika misingi yake, akisisitiza haja ya kuwepo sheria dhidi ya itikadi za Kiislamu. Kwa hivyo, ni wazi kabisa kwamba kwa mtazamo wa Macron, watu wenye msimamo mkali wa kushoto na kulia wanajaribu kuibua mvutano wa kidini nchini Ufaransa.
Kwa msingi huo, Rais wa Ufaransa amekosoa mitazamo ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo ya kushoto na kusisitiza kwamba, "wanawagawa watu kulingana na itikadi zao za kidini au jamii wanayotoka, na katika hali hii, mtaingia vitani na watu ambao hamuafikiani katika maadili na itikadi."
Hata hivyo makundi yenye mitazamo ya kufurutu mipaka yamepinga tahadhari ya Macron na kusema kwamba, sera za serikali yake ndiyo sababu ya migogoro ya Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni.
Katika mahojiano na televisheni ya "France 2", Jean-Luc Mélenchon, kiongozi wa mrengo wenye itikali kali wa kushoto, "La France Insoumise", amelaani matamshi ya Rais Emmanuel Macron na kusema kuwa, sera zake mwenyewe ndizo zilizosababisha machafuko ya ndani.
Alaa kulli hal, Macron alilivunja Bunge la Taifa la Ufaransa baada ya chama cha mrengo wa kulia kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya, na uchaguzi wa mapema wa Bunge la nchi hiyo umepangwa kufanyika Juni 30 na Julai 7.
Kwa hivyo basi, kwa mtazamo wa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuna uwezekano kwamba muungano wa mrengo wenye msimamo mkali wa Ufaransa na wanasiasa wenye itikadi kali walioshinda katika Bunge la Ulaya, utaimarisha makundi yenye mitazamo ya kufuru mipaka nchini Ufaransa na kuyumbisha usalama wa nchi hiyo.