Utawala wa Kizayuni wazuia kutolewa misaada kwa waliojeruhiwa kaskazini mwa Gaza
(last modified Mon, 04 Nov 2024 12:18:49 GMT )
Nov 04, 2024 12:18 UTC
  • Utawala wa Kizayuni  wazuia kutolewa misaada kwa waliojeruhiwa kaskazini mwa Gaza

Shirika la Ulinzi wa Raia wa Ukanda wa Gaza limetangaza hatua ya utawala katili wa Kizayuni ya kuzuia juhudi za kuwasaidia Wapalestina waliojeruhiwa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kanali ya Sahab leo Jumatatu, Shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza limetoa taarifa na kutangaza kuwa,  shughuli za shirika hilo kaskazini mwa ukanda huo zimesitishwa kutokana na mashambulizi ya moja kwa moja na uchokozi unaoendelea wa jeshi katili la  Utawala wa Kizayuni tangu siku 13 zilizopita, na kwamba maelfu ya watu wameachwa bila huduma za dharura na matibabu Gaza.

Taarifa ya shirika hilo huko Gaza inasema kuwa wanajeshi wa jeshi linalokalia kwa mabavu ardhi za Palestina (Isreal) wamewashambulia wafanyakazi wake na kuwanyang'anya magari yao pamoja na kuwalazimisha wengi wao kuhamia maeneo kusini, ambapo pia wafanyakazi 7 wa shirika hilo wametekwa nyara na Wazayuni.

Hospitali ya Al-Awda, iliyoko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, pia imetangaza kuwa tangu tarehe 5 Oktoba, hospitali hiyo haijapokea mafuta yoyote ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme unaohitajika hospitalini na kwamba kitengo cha huduma za dharura kwa wagonjwa hospitalini hapo pia kimefungwa kutokana na mashambulizi ya moja kwa moja ya utawala wa Kizayuni.

Hospitali hiyo imetangaza kwamba ili kutoa huduma kwa wagonjwa na majeruhi, kuna udharura wa kupokea mara moja dawa, makundi tofauti ya damu, chakula na maji.

Habari nyingine ni kuwa, walowezi wa Kizayuni wameushambulia mji wa Al-Bireh ulioko katikati mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan asubuhi ya leo na kuchoma moto idadi kubwa ya magari ya Wapalestina na kuharibu mengine kadhaa.

Vitendo hivyo vya kikatili vya utawala wa Israel na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, vinaripotiwa katika hali ambayo leo asubuhi, utawala huo, ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake dhidi ya Palestina na maamuzi ya jamii ya kimataifa, umefutilia mbali makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Knesset (Bunge) ya utawala wa Kizayuni, Jumatatu ya wiki iliyopita, ilipitisha sheria dhidi ya UNRWA  ambayo inapiga marufuku shughuli za UNRWA katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo bandia, tangu mwaka 1949.

UNRWA ndio uti wa mgongo wa usambazaji wa misaada ya kimataifa katika Ukanda wa Gaza, ambao sasa unakabiliwa na janga la kibinadamu lililosababishwa na jinai za kinyama za Israel.