Ethiopia yawapiga chanjo ya surua zaidi ya watoto milioni 11
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126780-ethiopia_yawapiga_chanjo_ya_surua_zaidi_ya_watoto_milioni_11
Ethiopia imeshawapiga chanjo watoto zaidi ya milioni 11 kama sehemu ya kampeni ya taifa zima ya kudhibiti ugonjwa wa surua unaoendelea kulisumbua taifa hilo.
(last modified 2025-05-24T22:50:15+00:00 )
May 24, 2025 22:50 UTC
  • Ethiopia yawapiga chanjo ya surua zaidi ya watoto milioni 11

Ethiopia imeshawapiga chanjo watoto zaidi ya milioni 11 kama sehemu ya kampeni ya taifa zima ya kudhibiti ugonjwa wa surua unaoendelea kulisumbua taifa hilo.

Kampeni ya chanjo, ambayo imekusudiwa kuwapiga chanjo watoto milioni 17.5 wenye umri wa kati ya miezi tisa hadi miaka mitano, inafanyika hivi sasa katika maeneo yote ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Fana Broadcasting Corporate ambalo limenukuu taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa na maafisa wa Wizara ya Afya wa Ethiopia.

Ripoti hiyo aidha imesema: "Mpango wa chanjo si tu unalenga kuwalinda watoto kukabiliana na ugonjwa wa surua, lakini pia ni kwa ajili ya kuwatambua wale walioko katika hatari kutokana na utapiamlo, upungufu wa vitamini A na mapungufu katika chanjo ya kawaida."

Surua ni ugonjwa wa virusi unaoambukiza sana hasa watoto. Unaenezwa kupitia matone yanayotoka wakati mgonjwa anapopumua na wakati mgonjwa anapogusana moja kwa moja na mtu mwingine.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa wa surua bado haujadhibitiwa nchini Ethiopia na kesi mpya zinaendelea kuripotiwa kila mwaka. 

Ugonjwa huo huathiri zaidi watoto wadogo na unaweza kusababisha matatizo makubwa kama vile homa, kikohozi kikavu, kuvuja mafua puani na kujaa makohozi kooni. Unaweza kuzuilika kupitia chanjo inayopigwa kwa wakati mwafaka.