Kamandi ya Majeshi la Iran: Uchokozi wowote utakabiliwa na jibu kali
Vikosi vya Jeshi la Iran vimetoa taarifa vikisisitiza kuwa, vitatoa majibu thabiti dhidi ya vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.
Kamandi ya Majeshi la Iran ilitoa taarifa hiyo jana Ijumaa kwa ajili ya kuadhimisha kumbukizi ya kukombolewa mji wa Khorramshahr ulioko kusini magharibi mwa Iran kutoka kwa utawala wa Baath wa Iraq mwaka 1982 na kubainisha kwamba, "Vikosi vya jeshi la Iran vitajibu kwa nguvu na uwezo wake wote tishio lolote au hatua yoyote ghalati ambayo inalenga malengo na thamani tukufu za Mapinduzi ya Kiislamu."
Taarifa hiyo imeendelea kusoma kuwa, Rais asiye na haya wa Marekani (Donald Trump) angefanya vyema zaidi kudurusu historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, Vita vya Kujihami Kutakatifu, na Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya 1 na 2 kabla ya kuzungumza juu ya Iran yenye fahari, ili kwa kiasi fulani apate kudiriki mahesabu yake yenye makosa.
Mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ilidhihirisha uwezo wake wa kijeshi kwenye Operesheni ya Ahadi ya Kweli I na II, yakiwa ni mashambulizi ya kulipiza kisasi kujibu uvamizi na uchokozi wa Israel.
Mnamo Mei 24, 1982, wanajeshi wa Iran waliukomboa mji wa Khorramshahr katika operesheni kubwa iliyopewa jina la Beit al-Muqaddas kutoka kwa utawala wa kidikteta wa Baath wa Saddam Hussein uliokuwa ukiungwa mkono na mataifa mengine.
Juzi Alkhamisi, Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri alionya pia kuwa, shambulio lolote dhidi ya Iran, litawasababishia hasara kubwa wavamizi na wala hawataweza kuambulia chochote.