Watu takribani 50 wafariki baada ya kuporomoka mgodi wa dhahabu Sudan
(last modified Sun, 29 Jun 2025 14:14:04 GMT )
Jun 29, 2025 14:14 UTC
  • Watu takribani 50 wafariki baada ya kuporomoka mgodi wa dhahabu Sudan

Takriban watu 50 wamefariki dunia kufuatia kuporomoka kwa mgodi wa dhahabu kaskazini mashariki mwa Sudan, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti Jumapili.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi katika jangwa la Howaid, katika Jimbo la Mto Nile, kwa mujibu wa gazeti la ndani la Alrakoba.

Mashuhuda walieleza kuwa kiasi kikubwa cha mchanga na mawe kiliporomoka juu ya wachimbaji waliokuwa wakifanya kazi kwenye eneo la mgodi wa kienyeji, linalojulikana kwa shughuli zisizo rasmi za uchimbaji.

Juhudi za uokoaji zilikumbwa na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa mashine nzito na vikosi maalum vya uokoaji, hali iliyochelewesha kutolewa kwa miili ya marehemu kutoka chini ya kifusi, waliongeza mashuhuda.

Katika eneo hilo hilo, tukio kama hilo lilitokea miezi miwili iliyopita na kusababisha majeruhi.

Janga hili limefufua upya ukosoaji dhidi ya ukosefu wa usimamizi wa serikali na miundombinu duni katika maeneo ya uchimbaji wa madini ya kienyeji, ambapo maelfu ya watu hufanya kazi katika mazingira hatarishi bila kuwa na usimamizi rasmi au viwango vya usalama.