Ripoti: Israel imevurumishiwa makombora 26,000 tokea Oktoba 7
(last modified Sun, 03 Nov 2024 06:44:37 GMT )
Nov 03, 2024 06:44 UTC
  • Ripoti: Israel imevurumishiwa makombora 26,000 tokea Oktoba 7

Makombora zaidi ya 26,000 yamevurumishwa kuelekea katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), tokea utawala huo wa Kizayuni uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba mwaka jana.

Kanali ya 12 ya utawala wa Kizayuni imetangaza katika ripoti yake kuwa, tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, maroketi na makombora 26,360 yamerushwa dhidi ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, makombora hayo yalirushwa dhidi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kutoka Ukanda wa Gaza, Lebanon, Iran na Yemen.

Israel ilishadidisha hujuma na vita vyake vya kikatili dhidi ya Gaza iliyozingirwa tokea tarehe 7 Oktoba, 2023, baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas kutekeleza operesheni isiyo na kifani ya Kimbunga cha al-Aqsa, dhidi ya utawala ghasibu unaoikalia Palestina kwa mabavu, kulipiza kisasi cha ukatili uliochupa mipaka wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Makomboya ya balestiki ya Iran yakielekea Tel Aviv

Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya mashambulizi hayo, utawala katili wa Israel umeshindwa kufikia malengo yake yaliyotangazwa ya kuiangamiza Hamas na kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza.

Tokea Oktoba 7 mwaka jana, utawala haramu wa Israel umeua shahidi Wapalestina zaidi ya 43,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.