Iran yalitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua za kukomesha jinai za Israel
(last modified Sat, 16 Nov 2024 12:33:25 GMT )
Nov 16, 2024 12:33 UTC
  • Iran yalitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua za kukomesha jinai za Israel

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za lazima ili kukomesha jinai za utawala ghasibu wa Israel.

Amir Saeed Iravani amesema hayo katika barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akisisitiza kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za lazima ili kukomesha jinai za Israel na hatua yake ya kukiuka mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya Iran.

Balozi Iravani amesema uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa utawala ghasibu wa Israel, pamoja na kuzuia kwake kutekeleza majukumu Baraza la Usalama kama mwanachama wa kudumu, kumeufanya utawala huo kuwa na kiburi zaidi cha kuendeleza jinai na hujuma zake huko Gaza na Lebanon.

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia amesema: Kwa vile watawala wa utawala wa Kizayuni wanaona kubakia kwao ni kupanua vita hivyo na kuitumbukiza Marekani ndani yake, wanajaribu kuandaa njia ya kutokea mgogoro mpya kwa kutumia vibaya hali ya sasa ya kisiasa ya Marekani.