Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tutaendelea kuunga mkono Mhimili wa Muqawama
(last modified Mon, 18 Nov 2024 07:24:53 GMT )
Nov 18, 2024 07:24 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Tutaendelea kuunga mkono Mhimili wa Muqawama

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran itaendelea kuuunga mkono Mhimili wa Muqawama, serikali na wananchi wa Syria.

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, alitoa sisitizo hilo jana Jumapili alipokutana na Meja Jenerali Kifah Moulhem, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Syria na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendeleza uungaji mkono wake wa kistratejia kwa Syria katika kupambana na ugaidi na kueneza amani na utulivu nchini humo.
 
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Syria amepongeza msimamo wa kuheshimika wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuunga mkono Muqawama na akaeleza kuwa msimamo huo unaziimarisha na kuzitia nguvu nyoyo za wananchi wa eneo hili.

Katika mazungumzo hayo, pande mbili za Iran na Syria zimesisitiza juu ya kuimarishwa maelewan kati yao katika nyanja mbalimbali hususan katika nyanja ya ulinzi na usalama kwa lengo la kutokomeza ugaidi na kuendeleza ushirikiano katika kueneza amani na utulivu katika eneo.

 
Mapema jana, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, Waziri wa Ulinziwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana pia na Rais wa Syria Bashar Assad na wakajadili masuala ya ulinzi na usalama katika eneo na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kusambaratisha muundo wake kwa namna itakayosaidia kuleta utulivu na usalama katika eneo.
 
Siku ya Jumamosi, Waziri wa Ulinzi wa Iran akiongoza ujumbe maalumu, aliwasili Damascus, mji mkuu wa Syria, kuitikia mwaliko wa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo../