Kuongezeka kwa maandamano barani Ulaya dhidi ya jinai za Wazayuni
Kuendelea kwa jinai za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza na Lebanon kumepelekea kupanuka uungaji mkono kwa Palestina na chuki dhidi ya Wazayuni barani Ulaya.
Maelfu ya watu wa Ireland wameandamana mjini Dublin wakiwa na mabango yaliyokuwa na maandishi: "Sitisha Ufadhili wa Mauaji ya Kimbari" wakipinga uuzaji wa hati fungani ya dhamana ya vita (bondi) nchini humo.
Jamhuri ya Ireland ndiyo nchi inayouza hati fungani za vita za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Ulaya, na Benki Kuu ya Jamhuri ya Ireland imeteuliwa kuwa mamlaka yenye uwezo wa kuidhinisha hati hizo. Inasemekana hati hizo zinatumika kama wenzo ya kuunga mkono vita vya utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon. Itakumbukwa kuwa, mnamo Mei 2024, Jamhuri ya Ireland, Norway na Uhispania ziliitambua rasmi Palestina. Serikali ya Ireland pia ni moja ya nchi muhimu za Ulaya zinazokosoa zaidi jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon. Mwenendo huu wa Ireland wa kukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na uuzaji wa hati ya dhamana ya vita za utawala huo ghasibu unaonyesha siasa za undumakuwili na pengo kati ya sera iliyotangazwa rasmi na matendo ya serikali ya Ireland katika uhusiano wake na utawala huo katili wa Kizayuni.
Alice Mary Higgins, seneta wa kujitegemea wa Ireland, ameliambia shirika la habari la Anatolia kuwa: "Msaada wa Benki Kuu ya Jamhuri ya Ireland kwa utawala pandikizi wa Israel ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa." Seneta huyu ambaye ameshiriki katika maandamano yaliyofanyika huko Dublin ya kuwatetea Wapalestina, ameongeza kuwa: "Bondi hizi, ambazo hapo awali ziliuzwa na Uingereza, zililetwa Dublin baada ya Brexit na Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya. "Alice Mary Higgins" amesema kuwa: "Dublin haipaswi kuwa msaidizi au kusahilisha uhawilishaji wa fedha hizi au ununuzi wa silaha wa utawala pandikizi wa Israel.
Radiamali ya wananchi wa Ireland dhidi ya sera za undumakuwili za serikali yao wakipinga jinai za utawala wa Kizayuni inaonyesha kwamba, wananchi wanafahamu vyema sura halisi ya utawala wa Kizayuni unouawa watoto na wanawake huko Gaza, na misimamo ya kindumakuwili ya serikali za nchi za Ulaya. Zaidi ya siku mia nne 400 zimepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Utawala huo unaendeleza jinai zake kwa uungaji mkono kamili wa serikali za Magharibi. Himaya na uungaji mkono huo wa Magharibi kwa Israel vinatolewa kana kwamba utawala huo hajafanya jinai yoyote ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Serikali za nchi za Ulaya daima zimekuwa zikiuhami na kuusaidia kwa hali na mali utawala wa Kizayuni wa Israel, na pale zinapoukosoa utawala huo huwa ni hatua ya kimaonyeshi tu ya kutaka kujidhihirisha kuwa ni watetezi wa haki za binadamu kwa lengo la kuhadaa maoni ya umma, lakini kivitendo, hazichukui hatua yoyote dhidi ya utawala huo pandikizi. Pamoja na hayo yote, maandamano na ukosoaji mkubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni katika nchi za Ulaya na Marekani vinaonyesha kuwa, fikra za wananchi wa nchi za Magharibi zinaelewa sura halisi ya utawala wa katili wa Israel na sera za kindumakuwili za serikali za nchi za Magharibi kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Palestina.
Gazeti la The Guardian pia limeashiria suala la kutochukua hatua Wamagharibi mbele ya jinai na unyama wa Wazayuni na kuandika: “Uchambuzi wa Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa asilimia 70 ya waliouawa Gaza ni wanawake na watoto, wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miaka 5 na 9. Hadi kufikia Septemba mwaka huu, vitoto vichanga 710 vilikuwa tayari vimeuawa na jeshi la Israel huko Gaza. Hadi kufikia mwezi uliopita, Israel imeangamiza kabisa familia zisizopungua 902 huko Gaza. Kuanzia vitoto vichanga hadi wazee, wote wamefutwa milele kwenye daftari la usajili. Hata hivyo, hakuna takwimu yoyote kati ya hizo hapo juu liliyoyumba imani ya Wamagharibi (kwa utawala wa Kizayuni wa Israel)."