Kamanda wa IRGc asema Iran imejiandaa kwa kila hali, aionya Marekani
(last modified Thu, 29 May 2025 04:31:59 GMT )
May 29, 2025 04:31 UTC
  • Kamanda wa IRGc asema Iran imejiandaa kwa kila hali, aionya Marekani

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Meja Jenerali Hossein Salami, amepuuza vikali vitisho vya kijeshi kutoka Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisisitiza kuwa taifa hili limejiandaa kikamilifu kukabiliana na hatari yoyote, na lina uwezo wa kujilinda dhidi ya aina zote za vitisho.

Akizungumza Jumatano  katika mkutano uliofanyika mjini Hamadan, magharibi mwa Iran Meja Jenerali Salami amesema: Tunawaambia viongozi wa Marekani kuwa tuko tayari kwa kila hali. Taifa letu halitawahi kusalimu amri kwa matakwa ya kisiasa ya mataifa mengine. Vidole vyetu viko tayari kufyatua risasi, na tuko tayari kuwashambulia. Wakithubutu kufanya kosa, majibu yetu yatakuwa ya haraka na ya kuumiza kiasi cha kuwafanya wajutie siku hiyo."

Amesifu mshikamano wa wananchi wa Iran katika nyanja za kisiasa na wakati wa misukosuko, akisema kuwa raia wa Iran hufanya maamuzi sahihi wakati wa dharura na hubaki na umakini wa hali ya juu.

Aidha amesema:  "Katika kukabiliana na maadui, ni lazima tuelewe nguvu za kijeshi za adui pamoja na kina cha fikra na nia zao. Vita vya kisaikolojia ni moja ya mbinu zinazotumiwa na Marekani na washirika wake kujaribu kupenya katika fikra za jamii." 

Kamanda huyo mwandamizi amesisitiza kuwa majeshi ya Iran yako katika kilele cha uwezo wa operesheni na utayari wa kivita: "Tuko kwenye vita kamili , tunakabiliwa na vita vya kiuchumi, vikwazo, mashinikizo ya kisiasa ya kimataifa, upotoshaji mkubwa wa taarifa, propaganda kali kupitia vyombo vya habari, mashambulizi ya kiutamaduni, na vitisho mbalimbali kutoka kwa maadui walioko ndani na nje."

Jenerali Salami amesema licha ya vitisho vyote, Iran imesimama kidete, huku taifa likiendelea mbele kwa uthabiti, na kwamba wananchi wake hawatakubali kushinikizwa na matakwa ya kisiasa ya mataifa mengine.

"Tuna udhibiti wa juu katika nyanja za ulinzi, na tumekuwa tukijipatia nguvu za kukabiliana na mataifa yenye nguvu kubwa duniani."

Kamanda wa IRGC pia amepuuza matamshi ya vitisho kutoka kwa viongozi wa Israel dhidi ya Iran.

"Kwa mara nyingine nawatahadharisha, wakithubutu kufanya kosa lolote, tutawafungulia milango ya maangamizi bila kusita," ameongeza Salami.