Saudia, Qatar, UAE zamuonya Trump asithubutu kuanzisha vita na Iran
Tovuti ya habari ya Axios ya Marekani imeripoti kuwa, viongozi wa Saudi Arabia, Qatar, na Imarati (UAE) walipinga vikali shambulizi lolote dhidi ya Iran wakati walipoonana na Trump na kuonya juu ya madhara yake yasiyotabirika kwa washirika wa Marekani kwenye eneo hilo.
Shirika la Habari la Fars limenukuu taarifa ya tovuti hiyo ya Marekani na kutangaza jana (Alkhamisi) kwa kuandika: "Axios imetangaza habari hiyo ikinukuu vyanzo vitatu vya habari vikisisitza kuwa, wakati wa ziara ya hivi karibuni ya rais wa Marekani kwenye eneo la Asia Magharibi ambapo alizitembelea Saudi Arabia, Qatar na Imarati, nchi zote hizo tatu za Kiarabu zilipinga vikali mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na kumhimiza Trump kuendelea na mazungumzo na kufikia makubaliano mapya ya nyuklia na Iran."
Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), na baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi, ambayo yaliripotiwa kupinga makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 (JCPOA), hivi sasa yanaunga mkono mazungumzo yanayoendelea baina ya Iran na Marekani kuhusu kadhia ya nyuklia na kuondolewa vikwazo, kwa upatanishi wa Oman.
Tovuti ya habari ya Axios ya Marekani imeendelea kuripoti kwamba, viongozi wa nchi za Kiarabu za eneo hili wana wasiwasi kwamba waziri mkuu wa Israel anaweza kumtumbukiza Trump kwenye janga la kuingia vitani na Iran au Trump ataachana na mazungumzo na kufanya kosa la kuchukua hatua za kijeshi, hivyo walimuonya vikali asijaribu kuingia vitani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.