China yaibainishia Marekani mistari yake minne myekundu ambayo haipasi kuvukwa
(last modified Mon, 18 Nov 2024 02:36:02 GMT )
Nov 18, 2024 02:36 UTC
  • China yaibainishia Marekani mistari yake minne myekundu ambayo haipasi kuvukwa

Rais Xi Jinping wa China ameweka wazi mistari myekundu minne ambayo amesema haipasi kuvukwa na Marekani ili kuwepo uhusiano wenye usawa na sahihi kati ya nchi hizo mbili.

Xi amebainisha hayo katika mazungumzo na Rais Joe Biden wa Marekani waliyofanya jana Jumamosi pembeni ya kongamano la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) linalofanyika Lima, Peru, akisisitiza kuwa Beijing inalenga kukuza uhusiano "tulivu, sahihi na endelevu" na Washington.

Katika mazungumzo hayo, Rais wa China amefafanua kuwa, zikiwa ni nchi mbili kuu, si China wala Marekani inayopasa kumrekebisha mwenzake kulingana na utashi wake, kumkandamiza kwa kutumia kile kinachoitwa 'nafasi ya nguvu,' au kumnyima haki halali ya maendeleo kwa ajili ya kudumisha hadhi yake ya uongozi".

Xi ameendelea kueleza kuwa, Vita vipya Baridi havipasi kuanzishwa na kupiganwa na haviwezi kushinda, na akasisitiza kwa kusema: "kuidhibiti China si hatua ya busara, haikubaliki, na itaishia kushindwa."

Kiongozi huyo wa China ametilia mkazo pia umuhimu wa nchi hizo mbili kuamiliana kwa usawa.

Amekiri kuwa, tofauti kati ya mataifa makubwa haziepukiki, lakini ni muhimu kuheshimu baadhi ya maslahi ya msingi.

Mistari minne myekundu ambayo Xi ameibainisha kwa Biden ni suala la Taiwan, demokrasia na haki za binadamu, njia na mfumo unaofuatwa na China, na haki ya maendeleo ya China.

Rais wa China amesema mipaka hiyo minne haipasi kupingwa na kuvukwa; na ndiyo njia muhimu zaidi za kudhamini usalama katika uhusiano wa nchi yake na Marekani.

Japokuwa Marekani inafuata rasmi sera ya uwepo wa China Moja, na inaitambua Taiwan kama sehemu ya China licha ya kujitawala tangu mwaka 1949, lakini inaiunga mkono Taipei kwa kuiuzia silaha na kuahidi kuisaidia kijeshi endapo itashambuliwa na China, hatua ambayo kwa mtazamo wa Beijing ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya China.

Aidha, Rais wa China amesema katika mazungumzo yake na Biden kwamba nchi yake iko tayari kufanya kazi na serikali ijayo ya rais mteule Donald Trump.../