Bunge la Yemen: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Damascus ni jinai
Bunge la Yemen limelaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika mji mkuu wa Syria, Damascus na kuitaja hujuma hiyo ya Wazayuni kuwa ni jinai.
Bunge la Yemen limeitaja hujuma hiyo ya Israel kuwa imekiuka sheria za kimataifa na za kibinadamu.
Mtandao wa Sahab umelinukuu shirika la habari la IRNA na kuripoti kuwa, Bunge la Yemen jana lilitoa taarifa na kutangaza kuwa: Jinai za utawala wa Kizayuni za kuwashambulia raia zinaonyesha kutokuwa na uwezo wa kijeshi na kisiasa utawala wa Kizayuni na kushindwa kwa fedheha utawala huo kukabiliana na vikosi vya muqawama.
Bunge la Yemen limeongeza kuwa: Hujuma ya Israel dhidi ya Damascus, Syria ni jinai na imekiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo ya Kiarabu na imekanyaga sheria za kimataifa na za kibinadamu.
Katika kuendeleza hujuma zake dhidi ya Syria, utawala wa Kizayuni Alhamisi na Ijumaa ya juzi ulishambulia viunga vya Damascus.
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetangaza kuwa makamanda wake wawili wameuawa shahidi katika ujuma hiyo ya utawala wa Kizayuni huko Damascus.