Kupasishwa azimio jipya la Umoja wa Mataifa la kuwaunga mkono Wapalestina
Kamati ya Haki za Binadamu na Masuala ya Kibinadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imepasisha azimio na kusisitiza kuwa wananchi wa Palestina wana haki ya kujiainishia mustakbali wao katika ardhi za Palestina, na kwamba wana haki ya kuwa huru, kujitawala na kujikomboa haraka kutoka katika makucha ya ukaliaji mabavu wa utawala wa Kizayuni.
Kamati ya Haki za Binadamu na Masuala ya Kibinadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia imesisitiza kuhusu hukumu ya Mahakama ya The Hague kwamba hatua za kujitanua na uvamizi za utawala wa Kizayuni ni kinyume cha sheria na kutilia mkazo kukomeshwa haraka iwezekanavyo kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina. Azimio hili tajwa limepasishwa kwa kura za nchi 170, na ni nchi 5 tu yaani Marekani, Argentina, Paraguay, Micronesia na Nauru pamoja na utawala wa Kizayuni ndizo zilipiga kura ya kupinga azimio hilo.
Azimio jipya la Umoja wa Mataifa limepasishwa katika hali ambayo Israel ingali inaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Utawala wa Israel hukuu ukiendelea kupuuza na kukanya misingi yote ya kibinadamu na matakwa ya kimataifa si tu kuwa unaendelea kuvamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina bali unaendeleza pia mauaji ya kimbari dhid iya Wapalestina.
Kwa mara kadhaa sasa Umoja wa Mataifa umepasisha azimio kwa akthari ya kura za wanachama wa umoja huo ukitaka kuhitimishwa ukaliaji mabavu wa Israel na kutambuliwa rasmi haki ya wananchi wa Palestina ya kujiainishia mustakbali wao katika ardhi za Palestina; hata hivyo mara hii pia azimio hilo limepingwa na Israel na mshirika wake mkuu yaani Marekani na nchi kadhaa vibaraka.
Pamoja na hayo, licha ya upinzani wa Marekani na waitifaki wake, kupasishwa azimio hilo na nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa kunaonyesha takwa la dunia la kuhitimishwa ukaliaji mabavu wa utawala wa Kizayuni na kutambuliwa rasmi haki ya wananchi wa Palestina kwa ardhi yao.
Nawaf Salam Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya mjini Hague Uholanzi hivi karibuni alitetea haki ya kihistoria ya taifa la Palestina ya kuunda nchi yao huru na yenye umoja na kusema: 'Ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni ardhi zenye umoja, zilizo na mamlaka ya kujitawala na zilizoungana ambazo lazima ziheshimiwe.'
Kwa hakika, kupasishwa azimio jipya la Umoja wa Mataifa la kuunga mkono haki ya Wapalestina kujitawala, kwa mara nyingine tena kunaonyesha kuwa, utawala wa Israel licha ya jitihada zote na kuungwa mkono kwa pande zote na Marekani si tu umeshindwa kuishawishi jamii ya kimataifa iunge mkono hatua zake za kujitanua na kughusubu ardhi za Palestina, bali upinzani dhidi ya sera, vita vya Gaza na mauaji ya kimbari ya Israel umeongezeka duniani kote. Suala ambalo limezidisha pia malalamiko na ukosoaji kutoka kwa waitifaki wa Magharibi wa Israel ikiwemo Marekani.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Harvard John Mearsheimer anaandika kuhusu suala hili kwamba: Sera za uungaji mkono na ukingiaji kifua za Marekani kwa Israeli si tu kuwa zinahatarisha maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo bali pia kuendelea kwa sera hii tajwa kunaweza kusababisha kutengwa pakubwa Marekani duniani.
Jinai zisizo na kikomo wala hesabu za Israel dhidi ya Wapalestina, unyakuzi wa ardhi zao, na hatua ya Israel ya kupuuza matakwa ya kimataifa kumezifanya nchi za dunia kuzingatia pakubwa haki ya Wapalestina ya kujiainishia mustakbali wao na nchi hizo kutambua rasmi nchi huru ya Palestina; na kupasishwa maazimio mbalimbali katika uwanja huu kunathibitisha wazi suala hilo.