Al-Nujaba: Tutapiga kambi za US, ikiisaidia Israel kuishambulia Iraq
(last modified Sun, 03 Nov 2024 06:17:46 GMT )
Nov 03, 2024 06:17 UTC
  • Al-Nujaba: Tutapiga kambi za US, ikiisaidia Israel kuishambulia Iraq

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq amesema, kundi hilo la Muqawama litalenga kambi na vituo vya kijeshi vya Marekani endapo Washington itatoa msaada wowote katika mashambulizi yanayoweza kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iraq.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Haidera al-Lami amesema katika mahojiano na chombo kimoja cha habari kwamba, kundi hilo litajibu shambulio lolote litakalofanywa kutokea kambi za Marekani na Israeli dhidi ya nchi yake.

Kiongozi huyo wa Harakati ya Al-Nujaba amepuuzilia mbali vitisho vya hivi karibuni vya utawala wa Kizayuni akisisitiza kuwa, "Vitisho vya Israel vya kulenga Muqawama wa Iraq havitutishi."

Al-Lami amebainisha kuwa, "Lengo letu ni kuwaunga mkono Wapalestina na mashambulizi yetu dhidi ya walengwa wa Kizayuni yataisha pale tu utawala huo utakapoacha kushambulia Gaza."

Wanamuqawama wa Iraq

Katika wiki na miezi kadhaa iliyopita, Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq, muungano wa mirengo ya Muqawama, umeshambulia sehemu nyeti na muhimu za utawala wa Kizayuni huko Eilat, ulioko kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hivi karibuni pia, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Al-Nujaba ilisisitiza kuwa, vita dhidi ya wavamizi wa Kimarekani vitaendelea hadi itakapohakikishwa hakuna hata mwanajeshi mmoja wa Marekani aliyesalia katika ardhi ya Iraq.