Jun 30, 2024 02:16 UTC
  • Human Rights Watch: Waliouawa katika maandamano ya Kenya wanakaribia 30

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, karibu watu 30 wameaga dunia katika maandamano ya wiki hii ya kupinga muswada wa fedha wa 2024 ambao unaongeza ushiru wa bidhaa.

Taarifa iliyotolewa na Human Rights Watch inasema kuwa, maafisa wa usalama waliwafyatulia risasi waandamanji siku ya Jumanne ya tarehe 25 ya mwaka huu wakiwemo waandamanaji waliokuwa wakiwatoroka polisi.

Licha ya kwamba hakuna idadi rasmi ya watu waliouwa jijini Nairobi na miji mingine ya Kenya katika maandamano hayo, lakini Human Rights Watch imebaini kwamba karibu watu 30 waliuawa siku hiyo ya maandamano kwa mujibu wa taarifa iliopo kutoka kwa umma, takwimu kutoka hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti jijini Nairobi.

Otsieno Namwaya, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika kanda ya Afrika Mashariki ametoa wito kwa mamlaka nchini Kenya kuwaeleza maafisa wake wa polisi kwamba, wanastahili kuwa wanawalinda raia wanaondamanama kwa amani na kwamba vitendo vya kihuni vya polisi havikubaliki.

 

Siku ya Ijumaa Mahakama Kuu ya Kenya ilitoa agizo la kuzuia polisi ya kitaifa kutumia maji ya kuwasha, mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na za mpira pamoja na silaha nyengine dhidi ya waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha wa mwaka wa 2024.

Mashirika ya kiraia yametangaza kuwa, watu 53 wameshauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo huku jiji la Nairobi likiripoti vifo 30.

Waandamanaji hao wa Kenya sasa wanamtaka Rais wa nchi hiyo, William Ruto, ajiuzulu licha ya uamuzi wake wa kuuondoa muswada tata wa fedha wa 2024 uliokuwa umedhamiria kuongeza ushuru ili kusaidia kupunguza mzigo wa madeni nchini humo.