Jul 02, 2024 04:10 UTC
  • Chama tawala Australia chamwadhibu mbunge wa kike anayevaa hijabu kwa kuunga mkono dola huru la Palestina

Chama tawala cha Labour nchini Australia kimeamua kumfukuza mwakilishi Fatima Byman kutoka kwenye kundi lake la Baraza la Seneti kwa muda usiojulikana kwa sababu ameunga mkono pendekezo la Chama cha Kijani la kutambua rasmi Palestina kama taifa huru.

Ripoti iliyochapishwa na ABC News nchini Australia imesema uungaji mkono wa Byman kwa juhudi za kulitambua taifa huru la Palestina umezua utata ndani ya Chama cha Labour.

Chama hicho kimetangaza kuwa haki ya Byman ya kushiriki katika mikutano ya kundi la Seneti imesimamishwa kwa muda usiojulikana na Waziri Mkuu wa Australia ambaye pia ni kiongozi wa chama Anthony Albanese.

Tarehe 25 Juni, baraza hilo lilikataa kwa mara ya pili pendekezo lililowasilishwa na Chama cha Kijani la kutambua rasmi taifa la Palestina.

Mnamo mwaka wa 2022, Fatima Byman alikuwa mbunge wa kwanza anayevaa hijabu nchini Australia, na ndiye pekee aliyeunga mkono pendekezo la kulitambua taifa la Palestina kutoka Chama cha Labour; kwa sababu hiyo amepigwa marufuku kushiriki katika mkutano wa baraza la chama mwanzoni mwa mwezi Julai.

Kwa mwezi wa tisa mfululizo, jeshi la utawala haramu wa Israel linaendeleza vita vya maangamizi ya kizazi dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, ambavyo hadi sasa vimeua shahidi Wapalestina karibu elfu 40 na kujeruhi wengine 86,000 - wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Mashambulizi hayo pia yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na makazi ya raia.