Jul 02, 2024 04:13 UTC
  • Mkurugenzi wa Hospitali ya al Shifa: Niliteswa vikali katika magereza ya Israel

Mkurugenzi wa Hospitali ya al Shifa katika Ukanda wa Gaza ambaye alikuwa anashikiliwa na utawala wa Israel kwa zaidi ya miezi 7 amesema kuwa alikuwa akiteswa vikali ndani ya magereza ya Israel.

Mohammed Abu Salmiya ni miongoni mwa Wapalestina zaidi ya 50 walioachiwa huru na utawala wa Israel na kurejea Gaza. Salmiya aliwaambia waandishi wa habari  jana kwamba wafungwa katika magereza ya utawala wa Kizayuni wanakumbana na aina zote za mateso.

Abu Salmiya kabla  ya kuzungumza na waandish wa habari 

"Wafungwa wanateswa kila siku na kupigwa magerezani", amesema Mkurugenzi wa Hospitali ya al Shifa ya Ukanda wa Gaza aliyeachiwa huru kutoka garezani na utawala wa Israel. 

Ameongeza kuwa, wafungwa kadhaa waliaga dunia katika vituo vya usaili na walikuwa wakinyimwa chakula na dawa za matibabu. Mohammed Abu Salmiya ameongeza kuwa walinzi wa jela za utawala wa Israel wamemvunja kidole chake na kusababisha damu kuvunja kichwani kutokana na kipigo alichopata kwa kuwa walinzi hao wa Kizayuni walikuwa wakitumia marungu na mbwa kumpiga. 

Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Gaza imearifu kuwa, wanajeshi wa Israel wamewateka nyara Wapalestina wasiopungua 5,000 tangu mwezi Oktoba mwaka jana wakati jeshi la utawala huo ghasibu lilipoanzisha vita vya kikatili vya umwagaji damu na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza walio chini ya mzingiro. Imesema, hatima ya wafungwa wengi wa Kipalestina au kuhusu hali zao za kiafya haijulikani.