Jul 02, 2024 04:11 UTC
  • Malik Agar: Kuporomoka kwa Sudan ni hatari kwa nchi zote za kanda hii

Malik Agar, Makamu wa Rais wa Baraza la Utawala wa Sudan, ameonya juu ya hatari ya kuporomoka kwa Sudan, ambayo haitakuwa kwa nchi hiyo pekee, bali athari zake mbaya zitaenea katika nchi jirani na kwingineko.

Malik Agar amechora mandhari ya kutisha ya uwezekano wowote kugawanyika au kusambaratika Sudan kutokana na vita vya ndani, na akasema kwamba kutokana na eneo lake la kijiografia na kidemografia, Sudan inaweza kuwa lango la kupanuka na kusambaa machafuko katika kanda hiyo nzima, iwapo itasambaratika.

Ili kuepusha hali hiyo, Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Utawala nchini Sudan amesisitiza kuwa kila mmoja anatakiwa kufanya kazi ili kuweka mazingira ya kumaliza vita na kufikiwa makubaliano ya amani baina ya pande husika.

Jenerali Abdel Fattah al Burhan (kulia) Hamdan Dagalo

Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais wa Baraza la Utawala wa Sudan anaamini kuwa kiongozi wa kundi la RSF linalopigana na jeshi la Sudan, Hamdan Dagalo, hana udhibiti wa vikosi vyake na kwamba neno la mwisho ni la upande unaomuunga mkono yaani Imarati (UAE).

Baada ya takriban miezi 15 ya vita, mapigano yanaendelea katika pande tofauti nchini Sudan bila kuwepo dalili za kufikiwa makubaliano ya kumaliza mzozo huo ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, na kuibua mgogoro mkubwa wa binadamu.

Tags