Jul 02, 2024 06:10 UTC
  • Shambulio la RSF laua watu 8 wa familia moja msikitini Sudan

Watu wanane wa familia moja wameripotiwa kuuawa katika shambulio linalodaiwa kufanywa na wapiganaji wa kundi la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) magharibi mwa Sudan.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, wanamgambo wa RSF jana Jumatatu walishambulia kwa maroketi msikiti mmoja ulioko katika kitongoji cha al-Tijaniyah, viungani mwa mji wa el-Fasher jimboni Darfur Kaskazini na kusababisha mauaji hayo.

Taarifa ya Kamati za Uratibu wa Mapambano (CRC) imeeleza kuwa, aghalabu ya watu wanane waliouawa jana ni watoto, na kwamba watu wengine 12 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. RSF haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na hujuma hiyo ya umwagaji damu.

Wapiganaji wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, wamezidisha mashambulizi dhidi ya el-Fasher, mji wa mwisho wa Darfur ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la Sudan linaloongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema, mashambulizi hayo ya RSF yanafanywa bila ya kutofautisha maeneo ya kijeshi na ya kiraia, bali hata hospitali nyingi zimeshambuliwa mjini hapo.

Baada ya takriban miezi 15 ya vita, mapigano yanaendelea katika pande tofauti nchini Sudan bila kuwepo dalili za kufikiwa makubaliano ya kumaliza mzozo huo ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, na kuibua mgogoro mkubwa wa binadamu.

Tags