Jun 14, 2024 02:13 UTC
  • Ijumaa, 14 Juni, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 7 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1445 Hijria mwafaka na tarehe 14 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo, tarehe 7 Dhulhija miaka 1331 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS, mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama, na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir", yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS). ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 288 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70. ***

Charles Augustin de Coulomb

 

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi al Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kuyakomboa maeneo hayo.  ***

 

Miaka 194 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 Rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za waliowengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya,Ayatullah "Seyyed Mostafa Mojtahed Kashani", mwanachuoni na mujahid mashuhuri, alifariki dunia. Alizaliwa Kashan, mojawapo ya miji ya kati ya Iran, katika familia ya wanazuoni, na alipata elimu yake  ya awali kutoka kwa baba yake. Kisha akaenda Isfahan nchini Iran na kisha Najaf huko Iraq kumalizia elimu yake ili kufaidika na elimu ya wanazuoni wengi zaidi, na hatimaye akaifikia cheo cha Ijtihad. Ayatullah Mostafa Kashani pia alikuwa na uwezo wa hali ya juu katika ushairi na aliandika mashairi kwa Kiajemi au Kifarsi na Kiarabu. Lakini sifa zake muhimu zaidi ni kupinga dhumla na kutetea haki. Msomi huyu  mkubwa alikuwa ni miongoni mwa wapinzani wa dhulma na waungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiktiba ya Iran na alipigana dhidi ya uingiliaji wa wakoloni wa Uingereza na Russia nchini Iran na Iraq. Kwa mfano, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na uvamizi wa Waingereza nchini Iraq, Ayatullah Seyyed Mustafa Kashani sio tu alitoa fatwa za jihad na wanachuoni wengine, bali pia alionekana kwenye medani za vita dhidi ya wakoloni. Mwanawe, Ayatullah Seyyed Abolghasem Kashani, pia alikuwa mmoja wa wapiganaji wakubwa dhidi ya ukoloni wa Uingereza, hasa wakati wa kutaifishwa kwa sekta ya mafuta ya Iran. ***

 

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita mto mrefu na mkubwa zaidi wa Asia wa Yangtze Kiang ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko ya kutisha. Mvua kali za msimu zilizonyesha zilisababisha mawimbi na mafuriko makubwa yaliyovunja kingo na mabwawa yote ya kandokando ya mto huo. Maji hayo yaligubika ardhi ya majimbo 8 ya China. Inasemekana kuwa tukio hilo kubwa liliathiri karibu watu milioni 50 wakiwemo waliopoteza maisha, kupoteza makazi, uharibifu wa mashamba, wale waliofariki dunia kutokana na maradhi ya aina mbalimbali na kadhalika. ***

Mto Yangtze Kiang

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 Miladia nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama vile Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges akaanza shughuli ya uandishi na taratibu akaanza kuandika kisa mashuhuri cha Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu wake, hakuweza kumaliza kuandika kisa hicho. Luis ameacha athari mbalimbali za vitabu ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.***

Jorge Luis Borges

 

Tags