IRGC yashambulia meli nyingine ya mafuta ya US Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137328-irgc_yashambulia_meli_nyingine_ya_mafuta_ya_us_ghuba_ya_uajemi
Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC kimetangaza habari ya kushambulia meli nyingine ya mafuta Marekani katika Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2026-03-13T03:57:16+00:00 )
Mar 13, 2026 03:57 UTC
  • IRGC yashambulia meli nyingine ya mafuta ya US Ghuba ya Uajemi

Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC kimetangaza habari ya kushambulia meli nyingine ya mafuta Marekani katika Ghuba ya Uajemi.

Idara ya Uhusiano Mwema ya IRGC imesema katika taarifa kuwa: Meli ya Marekani ya ‘Safe Sea' yenye bendera ya Marshall Islands, ikiwa moja ya milki za jeshi la kigaidi la Marekani, imepigwa (kombora) Kaskazini mwa Ghuba ya Uajemi baada ya kupuuza na kutoheshimu maonyo ya Kikosi cha Majini cha Jeshi la IRGC.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, "Meli za mafuta na vyombo vingine vya baharini vinavyofanya kazi katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Lango-Bahari la Hormuz, zinapasa kufahamu kuwa, ukosefu huu wa usalama umesababishwa na uchokizi na uvamizi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Idara ya Uhusiano Mwema ya IRGC imebainisha kuwa, iwapo meli hizo zinataka kudumisha usalama wao na wa mabaharia wao katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Lango-Bahari la Hormuz, zinapasa kuheshimu sheria na masharti ya vita yaliyotangazwa na Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kamandi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ya Khaatamul-Anbiyaa hapo awali ilionya kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasubiri kwa hamu kubwa kuthibiti kwa madai ya vikosi vya jeshi la Marekani vya kusindikiza meli za mafuta na kujikita kwenye Lango-Bahari la Hormuz.

Rais Donald Trump wa Marekani mpaka sasa ameshindwa kutekeleza vitisho vyake kwamba jeshi la Marekani litaishambulia Iran mara 20 zaidi ya mashambulizi ya sasa, iwapo Jamhuri ya Kiislamu itazuia meli za mafuta kupita katika Lango-Bahari la Hormuz.