Jun 30, 2024 03:04 UTC
  • Wanachama wa BRICS wasisitiza kupanua ushirikiano katika sekta ya kilimo

Naibu Waziri wa Jihad ya Kilimo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Kilimo wa nchi wanachama wa kundi la BRICS kuhusu kupanua ushirikiano kati ya nchi wananchama wa kundi hilo katika nyanja za kilimo.

Alireza Mohajer amesema kuwa, kustawisha ushirikiano kati ya nchi wanachama wa BRICS ni hatua chanya katika uwanja wa kupeana ujuzi na kubadilishana taarifa na tajiriba; na hiyo itakuwa njia ya kuboresha usalama wa chakula katika nchi wanachama wa kundi hilo.  

Mwakilishi wa Iran katika mkutano wa Mawaziri wa Kilimo wa BRICS uliofanyika Russia ameongeza kusema kuwa: Katika mkondo wa kupunguza taathira mbaya za mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na suala hilo, kuna ulazima wa kuhifadhi maliasili na bioanuwai, na kujikita katika mfumo wa uzalishaji wa kilimo wenye tija, thabiti na endelevu. 

Naibu Waziri wa Jihad ya Kilimo wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu  imetayarisha mazingira ya kupanua mitandao ya kibiashara katika sekta ya kilimo kieneo na kimataifa kupitia njia ya kushirikiana nchi wanachama wa BRICS kutokana na nafasi yake nzuri ya kijiografia na njia bora za usafirishaji.  

Mohajer ameeleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajaribu kuondoa vikwazo vilivyopo katika njia ya kustawisha ushirikiano wa kilimo kati ya wananchama wa BRICS.