Jun 28, 2024 15:09 UTC
  • Msemaji wa Tume ya Uchaguzi Iran: Muda wa kupiga kura uchaguzi wa rais umerefushwa

Msemaji wa Tume ya Uchaguzi nchini Iran amewaambia waandishi wa habari kwamba, muda wa kupiga kura katika uchaguzi wa rais ulioanza mapema leo kote nchini umerefushwa hadi saa nne usiku.

Mohammad Eslami, msemaji amewaambia waandishi wa habari kwamba, kwa idhini ya Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmed Vahidi, muda wa kupiga kura katika uchaguzi wa 14 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu umerefushwa hadi saa nne usiku. 

Duru ya 14 ya uchaguzi wa rais ilianza saa mbili kamili asubuhi Ijumaa ya leo - Julai 8 - katika vituo 58,640 vya kupigia kura kote nchini Iran.

Vilevile, vituo 344 vya kupigia kura vilitayarishwa katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya Wairani wanaoishi ng'ambo ili kumchagua Rais wa Serikali ya Awamu ya 14 katika balozi na vituo vya uwakilishi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi nyingine.

Wairani wasiopungua milioni 61 wametimiza masharti ya kupiga kura.

Wagombea wanne wanachuana kuwania kiti cha Urais kilichobakia wazi baada ya kufariki dunia aliyekuwa Rais wa Iran Shahidi Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta, tarehe 19 Mei mwaka huu.

Wagombea hao ni Saeed Jalili, mkuu wa zamani wa timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran, Muhammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge, Mostafa Pourmohammadi ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, na Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa afya.

Wagombea, uchaguzi wa rais nchini Iran

Wagombea wengine wawili, Alireza Zakani, ambaye ni Meya wa Jiji la Tehran na Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi mkuu wa Wakfu wa Mashahidi na Masuala ya Veterani jana walitangaza kujitoa katika mbio za kuwania urais.

Duru mbalimbali zinatabiri kuwa, ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya wagombea watatu ambao ni Saeed Jalili, Muhanmmad Baqer Qalibaf wa mrengo wa wahafidhina na Masoud Pezeshkian wa mrengo wa mageuzi.