Jun 29, 2024 02:26 UTC
  • Wajapani waandamana kupinga ukatili wa kingono wa jeshi la Marekani huko Okinawa

Wajapani wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Tokyo wakipinga unyanyasaji wa kingono na ubakaji wa wanajeshi wa Marekani katika kisiwa cha Okinawa kusini mwa Japan.

Ni baada ya kuripotiwa kesi mbili za ubakaji wa wanawake wa Kijapani uliofanywa na wanajeshi wa Marekani huko Okinawa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Masataka Okano, alikutana na balozi wa Marekani nchini humo, Rahm Emanuel, jana Ijumaa, akitaka hatua za kinidhamu zichukuliwe kutokana na mashambulizi na ubakaji huo, ambao umetokea ndani ya miezi ya Desemba mwaka jana na Mei mwaka huu na kufichuliwa hivi karibuni. 

Baada ya kufichuka uhalifu huo, Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japan, Yoshimasa Hayashi, amewaambia waandishi wa habari kwamba "Kesi za uhalifu zinazofanywa na wanajeshi wa Merekani zinasababisha wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa Okinawa, na hazipaswi kutokea." 

Wajapani wakipinga ukatili wa jeshi la Marekani

Kesi hizo zimefichuliwa siku chache tu baada ya kubainika kuwa afisa wa jeshi la Marekani mwenye umri wa miaka 25 huko Okinawa alishtakiwa mwezi Machi kwa kumbaka msichana mdogo wa Kijapani miezi mitatu iliyopita.

Uhalifu huo umesababisha wasiwasi na mvutano kati ya wakazi wa Ukinawa karibu na kambi za jeshi la Merekani katika mkoa huo.

Kesi ya kubakwa msichana huyo mdogo wa Kijapani inawakumbusha wakazi wengi wa Okinawa tukio la ubakaji uliofanywa na wanajeshi watatu wa Marekani mwaka 1995 dhidi ya mtoto aliyekuwa na miaka 12, jambo ambalo lilisababisha maandamano makubwa ya kupinga kuwepo wanajeshi wa Marekani kwenye kisiwa hicho.