Jun 28, 2024 03:22 UTC
  • Qaani: Raisi, Abdollahian walithibitisha kuwa Iran inaweza kuikabili Marekani

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesifu na kupongeza sifa za kipekee walizojipambanua nazo Shahidi Rais Sayyid Ebrahim Rais na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, kwa kuiunga mkono kambi ya muqawama na kukabiliana na ubeberu wa Marekani.

Brigedia Jenerali Esmail Qaani alisema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa Arubaini ya Sayyid Ebrahim Raisi, ambaye alikufa shahidi na waziri wake wa mashauri ya kigeni, Hossein Amir-Abdollahian pamoja na maafisa wengine walioambatana nao katika ajali ya helikopta mnamo Mei 19. 

Jenerali Qaani amesema kauli na vitendo vya Mashahidi hao wa Iran vinatoa ithibati kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina uwezo wa kukabiliana na madola makubwa yenye nguvu, na wakati huo huo kuyafanya madola hayo yatengwe kimataifa, kama ilivyotengwa sasa Marekani.

Qaani amebainisha kuwa, jitihada za shakhsia hao wawili wa Kiirani katika uga wa kimataifa zilikuwa athirifu, na zimeweza kuimarisha nafasi na mamlaka ya Iran mkabala wa utawala unaoua watoto wa Israel, na muitifaki wake mtenda jinai, Marekani.

"Shakhsia hawa (Mashahidi Raisi na Abdollahian) walikabiliana na Marekani, na kutoa hakikisho kuwa mambo yanaweza kufanywa bila kuitegemea Marekani," ameongeza Jenerali Qaani.

Mashahidi Raisi na Abdollahian

Brigedia Jenerali Qaani  amesema Jamhuri ya Kiislamu itafanya kila iwezalo kuiunga mkono Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na makundi mengine ya muqawama katika mapambano ya kihistoria dhidi ya adui Mzayuni.

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH amebainisha kuwa, makundi ya muqawama yamestawi hatua kwa hatua na leo hii nguzo zote za kambi ya mapambano katika ngazi ya kikanda zinapambanua mambo na kujichukulia maamuzi.

 

Tags