Magaidi 13 wa al-Shabaab wauawa katika operesheni ya jeshi Somalia
(last modified Fri, 11 Jul 2025 15:55:09 GMT )
Jul 11, 2025 15:55 UTC
  • Magaidi 13 wa al-Shabaab wauawa katika operesheni ya jeshi Somalia

Shirika la kitaifa la ujasusi na usalama la Somalia (NISA) jana Ijumaa lilisema kuwa lmeifanya operesheni tatu zilizoratibiwa katika eneo la Shabelle ya Kati, na kuua takriban wanachama 13 wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, wakiwemo wapiganaji na makamanda wake.

Operesheni hizo za alfajiri ya Ijumaa zililenga mikusanyiko ya magaidi hao walipokuwa wamekusanyika kwa shabaha ya kuhamasishana. Mahema na hifadhi za silaha zilizokuwa zimefichwa chini ya miti ziliharibiwa.

Shirika hilo la usalama limesema operesheni ya kwanza katika kijiji cha Raage Elle iliua magaidi wanne, huku watano wakiuawa katika operesheni ya pili katika maeneo ya Hawaala-kulan na Reydableey.

Taarifa ya Shirika la kitaifa la ujasusi na usalama la Somalia imeongeza kuwa, operesheni ya tatu ilifanyika katika mji wa El-Baraf, ambapo magaidi wanne walitokomezwa.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya kikosi maalum cha Danab cha Jeshi la Somalia kuwaua zaidi ya wanamgambo 37 wa kundi la al-Shabaab katika kijiji cha Maqooqaha, kilichoko magharibi mwa Buulo Xaaji katika eneo la Lower Jubba, kusini mwa nchi.

“Mapambano dhidi ya al-Shabaab yataendelea kwa nguvu katika kila upande,” imesisitiza Wizara ya Ulinzi ya Somalia. Al-Shabaab imekuwa ikipigana na serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16 sasa, na mara nyingi huwalenga maafisa wa serikali na wanajeshi.