Jun 29, 2024 02:16 UTC
  • UN: Maelfu ya watu Sudan Kusini wanakabiliwa na janga la uhaba wa chakula

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, Sudan Kusini inakabiliwa na janga la ghasia, mafuriko, mgogoro wa kiuchumi na njaa, huku watu 79,000 katika Jimbo la Jonglei pekee wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema hayo katika ripoti yake mpya na kuzilaumu nchi wafadhili kwa kutotoa misaada inayohitajika ya kuweza kufanikisha kazi za kukabiliana na hali hiyo mbaya huko Sudan Kusini.

Sehemu moja ya taarifa ya OCHA imesema: "Kwa ujumla, zaidi ya watu milioni 7 nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na uhaba wa chakula na hilo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka 2023."

Taarifa hiyo pia imsema: "Idadi ya watu wanaokabiliwa na hali mbaya iitwayo IPC 5 ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha njaa katika Jimbo la Jonglei huko Sudan Kusini inatarajiwa kuongezeka karibu mara mbili hadi mwezi ujao wa Julai.

Ofisi hiyo pia imesema kuwa, Sudan Kusini inajiandaa kwa mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanakusudia kutoa msaada kuanzia mwezi Septemba, kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu milioni 2.4 kati ya milioni 3.3 wanaotarajiwa kuathiriwa na mafuriko hayo katika maeneo ya kaskazini, kaskazini mashariki na katikati mwa Sudan Kusini.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) pia imesema kuwa, msaada wa dola milioni 264 unahitajika lakini ufadhili ni duni na pande nyingi zimeshindwa kutekeleza ahadi zao za misaada.